Ofa ya TANAPA: Watanzania 6,368 watembelea Hifadhi za Taifa

|
Watanzania wakiangalia Wanyama pori

Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa nchini (TANAPA) imesema  Watanzania 6,368 wametembelea hifadhi za Taifa nchini kufuatia uamuzi wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira kwa kushirikiana na Wizara ya Utalii kuruhusu watanzania kuingia kwenye hifadhi za wanyamapori nchini bila kiingilio “OFA” kwa kipindi cha siku tatu kuanzia 2 – 4 Juni 2017, kama sehemu ya kuadhimisha siku ya mazingira Duniani.

Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara Mkoani Arusha iliongoza kwa kupokea wageni 1,582  ikifuatia na hifadhi ya Serengeti mkoani Mara wageni 1,085 na mikumi mkoani Morogoro wageni 1,004.

Hifadhi zilizopokea wageni wachache ni Kitulo mkoani Mbeya wageni 13, Mkomazi mkoani Kilimanjaro na Tanga wageni  43 na Gombe, Kigoma wageni 66.

Kwa hifadhi zilizotembelewa na wageni wengi uwepo wa miundombinu mizuri hususani ya barabara zinazopitika muda wote nje ya hifadhi imekuwa sababu kubwa ya hifadhi hizo kutembelewa na wageni wengi, huku zile zenye changamoto ya barabara  hususani za majini kupokea wageni wachache.

Ofa hiyo iliyotolewa kuadhimisha siku ya mazingira duniani ilijumuisha msamaha wa ada ya kiingilio na ada ya magari ya abiria na ilihusu kuvinjari kwa muda wa siku moja.

 

Maisha
Maoni