Test
Ofa ya TANAPA: Watanzania 6,368 watembelea Hifadhi za Taifa

Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa nchini (TANAPA) imesema  Watanzania 6,368 wametembelea hifadhi za Taifa nchini kufuatia uamuzi wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira kwa kushirikiana na Wizara ya Utalii kuruhusu watanzania kuingia kwenye hifadhi za wanyamapori nchini bila kiingilio “OFA” kwa kipindi cha siku tatu kuanzia 2 – 4 Juni 2017, kama sehemu ya kuadhimisha siku ya mazingira Duniani.

Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara Mkoani Arusha iliongoza kwa kupokea wageni 1,582  ikifuatia na hifadhi ya Serengeti mkoani Mara wageni 1,085 na mikumi mkoani Morogoro wageni 1,004.

Hifadhi zilizopokea wageni wachache ni Kitulo mkoani Mbeya wageni 13, Mkomazi mkoani Kilimanjaro na Tanga wageni  43 na Gombe, Kigoma wageni 66.

Kwa hifadhi zilizotembelewa na wageni wengi uwepo wa miundombinu mizuri hususani ya barabara zinazopitika muda wote nje ya hifadhi imekuwa sababu kubwa ya hifadhi hizo kutembelewa na wageni wengi, huku zile zenye changamoto ya barabara  hususani za majini kupokea wageni wachache.

Ofa hiyo iliyotolewa kuadhimisha siku ya mazingira duniani ilijumuisha msamaha wa ada ya kiingilio na ada ya magari ya abiria na ilihusu kuvinjari kwa muda wa siku moja.

 

Gari lisilo na dereva kufanyiwa majaribio hadharani Uingereza

Umma wa Uingereza unajiandaa kushuhuda majaribio ya kwanza ya basi linalotembea bila dereva.

Kwa zaidi ya majuma matatu yajayo takribani watu 100 watasafiri kwenye basi hilo kupitia njia ya Greenwich, London.

Gari hilo ambalo husafiri mpaka maili 10 kwa saa (km 16.1 kwa saa) litakuwa linaongozwa na tarakilishi (komputa).

Hata hivyo, ndani yake kutakuwa na mtaalamu ambae atalizuia pale itakapohitajika.

Kampuni ya Oxbotica, iliyotengeneza gari hilo, inasema watu 5,000 wameomba kushiriki katika jaribio hilo.

"Watu wachache sana ndio wamewahi kutumia gari linalojiendesha lenyewe, hivyo jambo hili ni kuwafanya watu wengi washuhudie wenyewe,” Mtendaji mkuu wa kampuni hiyo aliiambia BBC.

"Tuna tarajia watu wengi wataunga mkono zoezi hili linalotoa nafasi kwao,

"Pia tunasubiri kuona ni kwa jinsi gani watu watalizungumzia gari hili watakaposafirishwa kutoka kituo A mpaka B.”

Gari hilo lina viti vinne vya kukaa watu, na halina usukani wala breki za miguu.