Test
Morata wa Real Madrid auaga ukapera

Huku kukiwa na uvumi unaoenea kuhusu mchezaji Alvaro Morata kuiacha klabu yake ya Juventus, Mwanasoka huyo ameweka pembeni masuala yake hayo na kurudisha akili yake mwishoni mwa wiki kwa kufunga ndoa na mchumba wake mjini Venice.

Morata amekuwa akihusishwa na uwezekano wa kuhamia katika Klabu ya Manchester United msimu huu wa Joto baada ya kuhangaika kuimarisha nafasi yake katika kikosi cha kwanza cha Timu yake ya Real Madrid akitokea klabu ya Juventus.

Mchezaji huyo mwenye miaka 24 inaripotiwa kuwa hana furaha chini ya Kocha wake  Zinedine Zidane, lakini muhispania huyo hakuruhusu sintofahamu hiyo kuzuia sherehe yake ya harusi jana mchana.

Morata na mchumba wake, Alice Campello, walishiriki kiapo chao cha ndoa katika kanisa la Basilica del Redentore huko Venice kabla ya kupanda boti iliyowapeleka katika mji  maarufu wa Canals.

Morata huenda akaondoka Madrid, huku Timu ya Manchester United na AC Milan zikionyesha kumuhitaji.

BINTI MFALME WA JAPAN AKUBALI KUACHA NAFASI HIYO AOLEWE

Mjukuu wa kike wa Mfalme Akihito wa Japan, Binti Mfalme Mako, amekubali kupoteza hadhi na haki zote za umalkia ili aweze kuolewa na mpenzi wake, waliyekutana tangu akiwa chuo kikuu.

Taarifa zilizotangazwa jana na kituo cha televisheni cha umma, NHK, juu ya uamuzi huo wa Binti Mfalme Mako zimeitikisa Japan nzima.

Magazeti, televisheni, redio na mitandao ya kijamii imeamka ikiwa na habari hiyo, huku uchumba rasmi ukitazamiwa kutangazwa wiki chache kutoka sasa.

Mchumba wake, Kei Komuro, ni kijana wa miaka 25 aliyewahi kupewa jina la “Mwanamfalme wa Bahari” katika mashindano ya kushajiisha utalii hivi karibuni.

Mwanamume huyo kutoka familia ya watu wa kawaida, amezungumza na waandishi wa habari muda mfupi uliopita, ambapo amekwepa kabisa kuzungumzia suala la uchumba, akisema kuwa atasema “pale tu muda utakapowadia.”

Habari za uchumba huu zimezuwa mashaka makubwa sio tu juu ya nafasi ya mwanamke kwenye ukoo wa kifalme, bali pia mustakabali wa ufalme huo, ambao kwa mara ya kwanza ndani ya karne mbili zilizopita utachukua hatua ya kumuondoa madarakani mfalme aliye hai katika wakati ambapo warithi wa kiume ni wachache.

Mako, ambaye pia ana umri wa miaka 25, ni binti mkubwa wa Mwana Mfalme Akishino, ambaye ni mtoto wa pili wa kiume wa Mfalme Akihito, na kama ilivyo kwa wanafamilia wote wa kike wa ufalme huo, anapoteza hadhi na haki yake ya kifalme kwa kuolewa na mtu wa kawaida, kutokana na sheria zao.

Hata hivyo, sheria hiyo haiwahusu wanaume, ambapo Akihito na wanawe wameowa watu wa kawaida, na ambao sasa ni sehemu ya ufalme.

WANAVIJIJI INDIA WAWAFUNGISHA NDOA VYURA ILI KUOMBA MVUA

Wanavijiji waliokata tamaa nchini India wawafungisha ndoa  vyura ikiwa ni jitihada za kuwalilia miungu yao iwaletee mvua.

Hali hiyo imekuja kutokana na ukame ulioikumba nchi hiyo upande wa Kaskazini.

Wanavijiji hao wa Udalgiri na Assam walikuwa wamevaa mavazi ya kupendeza wakati wa harusi hiyo ya  vyura.

Vyura hao nao waliogeshwa, kuvalishwa  mavazi na kupambwa na rangi za asili huku chura wa kike akizawadiwa mkufu wa dhahabu na wanavijiji hao.

Ndoa hiyo iliongozwa na Padri wa Kihindu na karamu kubwa iliandaliwa kwa walioshuhudia ikiwa ni jitihada za kuomba mvua kwa miungu.

Baadaye, vyura hao waliokuwemo ndani ya dimbwi la maji waliachiwa waondoke na kisha wanavijiji hao kuendelea na masuala ya  chakula.

“Tuliwaacha huru vyura waondoke zao, ili waweze kuishi maisha yao na kufikisha ujumbe wa miungu ya mvua."

“Tulihakikiksha vyura hao wanatoka vijiji tofauti, kiasi kwamba miungu ya mvua itasikia ombi letu,” alisema mmoja wa wanavijiji.
Maelfu ya wakulima Kaskazini mwa India hususani eneo la Assam wanakabiliwa na ukame mkubwa kwa takribani juma moja sasa, huku zao la mpunga likiathirwa vibaya.

PIPPA MIDDLETON AFUNGA NDOA NA MATTHEWS, NI MDOGO WAKE MKEWE PRINCE WILLIAM

Wageni waalikwa wakiwemo Mwana mfalme wa Cambridge na mkewe Kate leo, Jumamosi wamehudhuria harusi ya Pippa Middleton na mumewe James Matthews.

Pippa Middleton, 33, ni mdogo wa Kate ambaye ni Mke wa mwana mfalme William, alichumbiwa mwaka jana na Matthews mwenye miaka 41.

Bibi harusi huyo  aliwasili katika viwanja vya Kanisa la Mtakatifu Mark huko Englefield, Berkshire akiambatana na baba yake mzazi, Michael Middleton, saa Tano na robo asubuhi  kwa saa za Uingereza.

Kanisa alilofungia ndoa  Pippa haliko mbali sana na nyumbani kwa familia ya Middleton,huko  Bucklebury.

Ulinzi uliimarishwa katika eneo hilo na wakazi wake walitakiwa kuwa na vitambulisho kwa siku hii na kushauriwa kutoongea na vyombo vya habari.

Lakini hata hivyo wakati Bi harusi akiwasili alipokelewa na kelele za shangwe kutoka kwa wapenzi wa utawala wa kifalme takribani 100 na wenyeji waliokusanyika katika eneo hilo

Mwanamfalme Harry, Princess Eugenie na mchezaji na mshindi wa mara kadhaa katika mpira wa Tennis,  Roger Federer aliyeambatana na mkewe  Mirka ni miongoni mwa wageni waalikwa kanisani hapo.