Latest News
Theresa May akwaa kisiki kwa wenzake Ulaya

Viongozi wa Umoja wa Ulaya (EU) wamemwambia Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May kuwa mapendekezo yake ya kumsaidia kusukuma mbele mchakato wa kuachana na umoja huo kwa lengo la kuwashawishi wananchi wa Uingereza kuunga mkono, hayajawekwa wazi kiasi cha kumsaidia kwa sasa.

Badala yake viongozi hao 27 wamesema wataendelea kuitafakari mipango hiyo kuelekea Machi 29 mwakani ambapo hatua watakazozichukua viongozi hao zitawasilishwa wiki ijayo.

Hayo yamebainika leo wakatika viongozi wa nchi 27 wanachama wa EU walipokutana na Waziri mkuu wa Uingereza, Theresa May ambaye baada ya kunusurika kura ya kutokuwa na imani na uongozi wake kutoka kwa wabunge wa Chama chake cha Conservative, akaamua kwenda kuonana na viongozi wenzake wa EU ili kuhakikishiwa juu ya masuala yenye utata katika muswada wa Mkataba wa Brexit ili aweze kuwashawishi wananchi wa Uingereza kuunga mkono mpango huo.

Wamesema wanasita kusema kwamba hakutakuwa na mabadiliko ya maana katika mkataba wa kisheria unaoihusu Uingereza kuachana na Umoja wa Ulaya na kusema kuwa mkataba huo hauruhusu majadiliano mapya.

Mpango wa Brexit una wakosoaji wengi lakini suala moja ambalo halibadiliki, ni suala la udhibiti wa mpaka lililowekwa kisheria kati ya Ireland Kaskazini ambayo ni sehemu ya Uingereza na Ireland ambayo ni mwanachama wa EU.

Latest News
Magufuli afuta maagizo ya barua iliyobadili rangi ya Bendera ya Taifa
Rais John Magufuli amefutilia mbali barua yenye kumbukumbu Namba CHA. 56/193/02/16 iliyokuwa na Kichwa cha habari 'MATUMIZI SAHIHI YA BENDERA, NEMBO NA WIMBO WA TAIFA'.
 
Katika taarifa iliyosambazwa kwa vyombo vya habari, Rais Magufuli amesema ameamua kuifuta barua hiyo kwa kuwa limezua taharuki na kuongeza kuwa iwapo kunatakiwa mabadiliko basi suala hilo lifuate taratibu kwa sababu suala hilo ni la kitaifa badala ya uamuzi wa mtu binafsi.
 
"Mimi mwenyewe tangu nasoma shule hadi leo najua bendera ya Taifa ina rangi ya njano na siyo dhahabu, na rangi hiyo ya njano inawakilisha madini yote, siyo dhahabu pekee," ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya Rais Magufuli.
 
Rais Magufuli ameagiza Bendera ya Taifa, Nembo na WIMBO WA TAIFA viendelee kutumika kama ilivyokuwa awali na kuwataka watanzania kuendelea kuwa wazalendo, kuipenda nchi yao na kuitangaza popote walipo ilimradi wazingatie sheria na maslahi mapana ya Taifa.
Latest News
Serikali kujadiliana upya sakata la Kikokotoo

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Kazi na Vijana, Jenista Muhagama amesema tayari wameshapokea barua kutoka Shirikisho la Chama cha Wafanyakazi kuhusu kikokotoo kipya cha pensheni baada ya mtumishi kustaafu na hivyo wanapanga siku ya kukutana nao ili kufanya majadiliano huku akisistiza mazungumzo hayo lazima yazingatie taratibu za kisheria.

Suala la mafao linalotokana na kikokotoo kipya limeibua mitazamo tofauti kwa wadau mbalimbali wakiwemo wabunge, wasomi na hata vyama vya wafanyakazi huku wengi wakidai kuwa matumizi ya kikokotoo hicho kipya ni unyonywaji wa wastaafu.

Tamko hilo la waziri Jenista limetolewa leo kwa mara ya kwanza tangu kuzuka kwa mijaddala mbalimbali ambapo amesema wanapanga namna ya kukutana na shirikisho  hilo la Vyama vya Wafanyakazi ili kufanya majadiliano hayo lakini kwa kuzingatia sheria.

Waziri Jenista ametoa tamko hilo pembeni mwa mkutano wake na OSHA, uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Latest News
Kifo cha mtoto chamweka matatani mfanyabiashara

Polisi mkoani Kagera inamshikilia mfanyabiashara mmoja kufuatia kifo cha aliyekuwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kashai, Manispaa ya Bukoba ambaye amehitimu elimu ya msingi mwaka huu.

Wakiongea na AZAM TV  baadhi ya wakazi  wa Mtaa wa Majengo Mapya  wamesema mwili wa marehemu ulikutwa ukining’inia juu ya lango kuu la nyumba ya mfanyabiashara huyo huku kichwa kikidaiwa kuning’inia  nje ambapo pia wamesema kabla ya kukutwa na umauti alikuwa akicheza na marafiki zake na baadaye alipotea katka mazingira ya kutatanisha.

Akizungumza na waandis wa habari, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Kamishina msaidizi, Revocatus Malimi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa wanamshikilia mfanyabiashara huyo kwa uchunguzi zaidi.

Aidha Kamanda Malimi amewataka wakazi wa Kagera kuwa makini katika kipindi hiki cha kuelekea Sikuku za Chrismas na Mwaka mpya na kuwalinda watoto wao ambao wengi wao wako likizo.

Ghala ya Tume ya Uchaguzi DR Congo lateketea

Moto umezuka katika jengo la Tume ya Uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, zikiwa zimesalia siku kumi kabla ya kufanyika uchaguzi wa Rais ambao kampeni zake zimegubikwa na vurugu.

Tume ya uchaguzi CENI imethibitisha kutokea kwa moto huo na uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea huku ikiwatoa hofu Wakongo juu ya uchaguzi huo.

Moto huo umezuka baada ya watu kuuawa Jumatano katika mapigano na polisi kando mwa mkutano wa hadhara wa upinzani mashariki mwa Congo.

Mapigano yalizuka katika mji wa Kalemie, wa ziwa Tanganyika ambako mgombea urais wa upinzani Martin Fayulu alikuwa akiendesha kampeni zake.

Mkuu wa tume hiyo ya uchaguzi, CENI amesema moto huo umezuka majira ya saa nane usiku wa manane katika ghala ambalo vifaa vya uchaguzi vimehifadhiwa.

Naye mmoja wa shuhuda wa tukio hilo Amy Gaylor akisimulia amesema, moto huo ulitokea majira ya usiku wa manane katika stoo kubwa ya Tume hiyo Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

"Wakati huo ndiyo tulipoviita vyombo vinavyohusika ambao walikuja kuulizia hali ilivyokuwa. Kwa kweli hatujui nini hasa chanzo cha moto huu. "

Moshi mzito mweusi umeonekana katika anga la jiji la Kinshasa mapema leo asubuhi huku  

Chanzo cha moto huo kikiwa hakijafahamika mara moja na Tume imeatangaza kuanza kwa uchunguzi na kwamba uchaguzi huo utafanyika kama ulivyopangwa.

Burundi yamnyoshea kidole Rwanda, yataka mkutano maalumu wa usuluhishi

Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza amesema kuna mzozo wa wazi kati ya taifa lake na taifa jirani la Rwanda katika kinachoonekana kuwa kudorora zaidi kwa uhusiano baina ya mataifa hayo mawili.

Rwanda na Burundi zimekuwa na uhasama kwa muda sasa huku Burundi ikiituhumu Rwanda kwa kuhusika katika jaribio la kupindua Serikali yake mwaka 2015 ambalo lilishindwa.

Kwa mujibu wa BBC, Burundi imedai kwamba Rwanda iliwafadhili waliohusika na jaribio hilo na kwamba inatoa hifadhi kwao.

Hata hivyo Rwanda yenyewe mara kwa mara imekuwa ikikanusha tuhuma hizo.

Kwa mujibu wa vyonzo vya uhakika, Rais Pierre Nkurunziza amemwandikia barua Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Yoweri Museveni ambaye ni Rais wa Uganda akimtuhumu Rwanda kama adui ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

"Rwanda ndiyo nchi pekee katika ukanda huu ambaye ni mmoja wa wahusika wakuu katika kuvuruga uthabiti wa taifa langu na kwa hivyo siichukulii kama taifa mshirika, lakini kama adui wa nchi yangu," ilisema sehemu ya barua hiyo ambayo imeonesha kutiwa saini na Nkurunziza Desemba 4.

Kiongozi huyo ametaka uitishwe Mkutano maalum wa EAC kwaajili ya kujadili mzozo huo kati ya Rwanda na Burundi.

Viongozi wa mataifa ya jumuiya hiyo ambayo kwa sasa inajumuisha nchi za Burundi, Rwanda, Uganda, Kenya, Tanzania na Sudan Kusini wamepanga kukutana Desemba 27 baada ya kushindwa kukutana mwishoni mwa juma lililopita kufuata Burundi kutoshiriki na kusababisha akidi kutotimia.

Mahakama Zambia yamsafishia njia Rais Lungu 2021

Mahakama ya Kikatiba ya Zambia imesema Rais wa sasa wa nchi hiyo, Edgar Lungu anazo sifa za kuwania nafasi hiyo tena katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2021.

Uamuzi huo wa Mahakama umetangazwa leo, Ijumaa na hivyo kutupilia mbali hoja ya wapinzani waliotaka Lungu asiwanie tena urais wakidai tayari ameshahudumu kwa awamu mbili kwa mujibu wa Katiba.

Wafuasi wa Chama cha Patriotic Front cha Rais, Edgar Lungu walifika mahakamani hapo wakiwa na shauku ya kutaka kujua uamuzi wa Mahakama hiyo mjini Lusaka.

Hata hivyo wengi wao walikuwa wamejawa na furaha tayari tangu awali kabla ya uamuzi huo kutolewa na  kunogeshwa zaidi na waliokuwa ndani ya Mahakama baada ya hukumu hiyo.

"Mahakama ya Kikatiba imeliweka vyema suala hili, imesema Rais Edgar Lungu anazo sifa za kuwania mwaka 2021."

"Hoja ilikuwa ni kwamba je vipindi viwili alivyovitumikia vinakamilisha awamu mbili za uongozi wake kwa mujibu wa Katiba? Jibu la Mahakama ni kwamba, si kweli."

Lakini ni nini kimetokea nchini Zambia?

Mwaka 2014 mwezi Oktoba Zambia ilimpoteza Rais wake wa Tano marehemu, Michael Charles Chilufya Sata aliyekuwa ameiongoza nchi hiyo kwa awamu moja kuanzia mwezi Septemba mwaka 2011.

Kutokana na kifo hicho uliitishwa uchaguzi wa mwezi Januari mwaka 2015 ambapo Edgar Lungu alishinda na kuhudumu kwa mwaka mmoja na nusu kabla ya uchaguzi mkuu wa mwezi Agosti mwaka 2016 ambapo alishinda tena na kuwa madarakani mpaka sasa.

Mwaka jana Lungu alitangaza rasmi kuwania uchaguzi wa mwaka 2021 na ndipo baadhi ya vyama upinzani na chama cha wanasheria wakaenda kwenye mahakama ya Katiba wakimpinga kwa hoja kuwa Rais huyo anavunja Katiba kwa kuwania awamu ya tatu.

Jaji wa Mahakama ya Katiba, Hildah Chibomba amesema urais wa awali wa Lungu wa mwaka mmoja na nusu hauwezi kuhesabiwa kuwa ni awamu iliyotimia.

Jiji la Dar es Salaam sasa kuongozwa na manaibu meya wawili

Hatimaye Jiji la Dar es Salaam, limefanikiwa kupata manaibu Meya wawili baada ya wagombea wawili kugongana kwa kupata kura 12/12.

Wawili hao waliogongana kura hizo baada ya kurudiwa mara kadhaa ni pamoja na mgombea wa CCM, Mariam Lulida, Diwani wa Kata ya Mchafukoge na Ally Harubu wa Kata ya Makumbusho kwa tiketi ya Chama cha CUF, ambao kutokana na kufungana huko, sasa wataongoza kwa kupokezana kwa miezi mitatu mitatu kuanzia Disemba 30.

Uchaguzi huo umefanyika katika ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam na hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa mkutano huo kufikia uamuzi huo na wawili hao wanachukua nafasi ya Mussa Kafana aliyekuwa Diwani wa Kata ya Kilawi CUF.