AfDB yaikopesha Serikali shilingi bilioni 589.3

|
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Doto James (kulia), akisaini mkataba wa Mkopo wa Masharti nafuu Wa shilingi bilioni 589.3 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Mwakilishi Mkazi wa Benki hiyo hapa nchini, Dkt. Alex Mubiru, (kushoto),

Serikali imesaini mikataba miwili ya mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 589.26 na Benki ya Maendeleo ya Afrika, AfDB kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Kabingo, Kasulu Manyovu yenye urefu wa kilometa mia mbili sitini kwa kiwango cha lami.

Hafla ya kusaini mikataba hiyo ilifanyika Hazina jijini Dar es Salaam na kuongozwa na katibu mkuu wa wizara ya fedha na mipango Doto James na mwakilishi mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, .

Katibu Mkuu Doto James amesema ujenzi wa barabara hizo ni sehemu ya kukamilisha miradi ya ujenzi wa barabara za kiwango cha lami nchini ili kutatua changamoto za kusafiri umbali mrefu.

Aidha Katibu mkuu huyo amesema kuwa utekelezaji wa mradi wa barabara wa Kabingo –Kasulu -Manyovu  ni sehemu ya mkakati wa Serikali ambao unalenga kuimarisha miundombinu ya usafiri ili kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kupunguza umasikini na kuimarisha ushirikiano wa kikanda.

"Barabara ya Kabingo-Kasulu-Manyovu ni kiunganishi muhimu katika maendeleo na uboreshaji wa biashara ndani na nje ya nchi.  Mradi wa ujenzi wa barabara hii utakwenda sambamba na ujenzi wa barabara ya Rumonge - Gitaza (kilomita 45) nchini Burundi ili kuboresha mtandao wa barabara za Afrika Mashariki." Alisisitiza James

Amesema pia kuwa mradi huo wa ujenzi wa barabara utakapokamilika utaunganisha Bandari ya Dar es Salaam na mikoa ya Magharibi mwa Tanzania na kufungua masoko ya kikanda nchini Burundi, Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

"Aidha, mradi utachangia katika kupunguza gharama za uendeshaji magari, kuboresha usalama wa barabara, kupunguza gharama zingine za usafirishaji  na  uboreshaji wa upatikanaji wa miundombinu ya huduma za kijamii na kiuchumi kwenye maeneo ya mradi mkoani Kigoma" alibainisha Doto James.

Dooto pia amebainisha kuwa mbali na mradi huo wa barabara , fedha hiyo pia itaboresha  Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ili kifikie hadhi ya kituo cha umahili wa usalama barabarani katika Kanda ya Afrika Mashariki ; Ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha Forodha katika Mpaka wa Manyovu (Tanzania) / Mugina (Burundi) na uboreshaji wa miundombinu ya huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na ukarabati wa masoko,  Usambazaji wa maji na usafi wa mazingira.

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Dkt. Alex Mubiru aliishukuru Serikali Tanzania kwa kutekeleza kikamilifu miradi inayofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika, na kuongeza kuwa mradi wa ujenzi wa barabara hiyo utaipa fursa za kiuchumi Mkoa wa Kigoma na nchi jirani ya Burundi.

Fedha
Maoni