Test
Rais Museveni akutana na kuteta na viongozi wa Kiyahudi

Viongozi wa makundi ya Kiyahudi kutoka nchini Marekani wamekutana na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni katika ziara yao ya siku mbili.

Wageni hawa ambao pia ni wafanyabiashara wakubwa duniani wapo Uganda kuangalia fursa zilizopo katika sekta mbalimbali wanakoweza kuwekeza.

Zaidi ya viongozi wa makundi hayo tofauti ya kiyahudi 20 wamewasili ikiwa ni neema kwa nchi ya Uganda huku ziara hiyo ikitarajiwa kufungua uhusiano mpya kati ya Uganda wageni hao hususan katika sekta ya biashara zao.

Uganda yenyewe kupitia Naibu waziri wake wa Mambo ya Nje ,Okello Oryem amesema ina matarajio makubwa katika ziara hiyo hususan kwenye masuala ya uwekezaji na teknolojia ambayo bila shaka wageni hao wana uzoefu ndani yake.

Naibu waziri huyo amesema, wamefurahishwa na ujio huo kutokana na ukweli kwamba mara nyingi mashirika ya utangazaji ya magharibi hayaongelei vizuri kuhusu Uganga hususan katika masuala ya usalama,uwekezaji na vivutio vilivyopo.

Waliokufa katika kampeni Nigeria wafikia 15

Idadi ya watu waliofariki dunia kwenye Kampeni za Mgombea wa Chama Tawala Nchini Nigeria, Muhammadu Buhari imeongezeka na kufikia watu 15 kutoka watu saba waliokufa siku ya kwanza kwa mkanyagano.

Duru za kitabibu zimebainisha idadi hiyo imeongezeka baada ya eneo hilo kufanyiwa usafi na kukutwa miili ya watu wengine saba waliohudhuria kwenye kampeni hizo za uchaguzi zilizofanyika siku ya Jumamosi.

Msemaji wa Hospitali ya Chuo Kikuu Cha Port Harcourt, Kem Daniel Elebiga amesema wamepokea jumla ya miili ya watu hao 15 waliokufa kwenye kampeni hiyo.

Amesema miili iliyopokewa ni ya wanaume watatu na wengine saba ni wanawake ambapo jumla ya watu waliojeruhiwa ni 12 na wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo.

Kampeni za lala salama zimeendelea kuwa kali ambapo upande wa Rais Buhari anaendelea kupambana kuhakikisha anarejesha tena kiti chake anachokishikilia.

Balozi wa Ethiopia nchini amwaga chozi mkoani Tanga

Balozi wa Ethiopia nchini Tanzania, Yonas Yoset Saube leo amejikuta akimwaga machozi katika Hospitali ya Rufaa ya mkoani Tanga, baada ya kushuhudia miili ya wahamiaji kutoka nchini mwake waliokufa tangu Novemba mwaka jana.

Balozi huyo amewasili mjini Tanga kwa ajili ya taratibu za mazishi ya wahamiaji hao baada ya Serikali ya Tanzania na Ethiopia kukubaliana kuwasitiri maiti hao mkoani humo.

Inadaiwa kuwa wahamiaji hao kutoka nchini Ethiopia walikumbwa na dhoruba wakiwa katika boti ndani ya Ukanda wa Bahari ya Hindi wakitokea nchini Kenya wakilenga kwenda kutafuta maisha katika nchi nyingine na kupelekea kupoteza maisha ya wahamiaji wanane kati ya 13 huko Mkinga mkoani Tanga.

Dunia yaadhimisha Siku ya Wapendanao

Wakati Dunia leo ikisheherekea siku ya wapendanao maarufu kama Valentine's Day, nchi mbalimbali zimesheherekea siku hii katika tamaduni zao na aina tofauti kulingana na jamii husika.

Licha ya Siku hii kuwa na historia ya kiimani lakini kwa sasa imegeuka kuwa siku ya familia, wapendanao na hata ya kibiashara.

Katika sehemu kadhaa duniani siku hii ya Valentine ambayo huadhimishwa kila Februari 14 imeshuhudiwa watu wakitumiana maua, marafiki na familia wakijumuika kwa chakula cha pamoja na hata kubadilishana zawadi.

Lakini kwa Tanzania kama zilivyo nchi nyingine, katika mitandao ya kijamii watu na marafiki mbalimbali wametakiana heri katika kusheherekea siku hii kwa kutumiana jumbe mbalimbali za upendo na wengine kutumiana zawadi zilizopambwa kwa rangi nyekundu.

Je kwa upande wako wewe leo umeiathimishaje siku hii?

Wakuu wa Majeshi Afrika wakubaliana kushughulikia uhalifu unaovuka mipaka

Viongozi wa Majeshi ya nchi za Afrika walikutana na kujadili juu ya Ushirikiano katika Sekta ya Usalama ikiwa ni Mpango Mkakati wa Kuzuia Uhalifu unaovuka mipaka ikiwemo uhalifu wa kimtandao na ugaidi.

Hayo yamesemwa na Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro baada ya kurejea nchini akitokea Rwanda ambako viongozi hao walikutana kujadili changamoto za ulinzi na usalama katika maeneo yao.

Akizungumza mara baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam, IGP Sirro amesema, katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na ongezeko kubwa la uhalifu wa kuvuka mipaka ambapo miongoni mwa tishio la uhalifu huo ni lile la mitandao ambalo limekuwa likisababisha wizi wa fedha kutoka nchi moja kwenda nyingine, sanjari na ugaidi ambao umesababisha kupoteza maisha ya wengi.

Amesema mbali na kukabiliana na kujadili matishio haayo ambayo mengi yamekuwa yakitokea kwa nchi nyingine lakini pia wamekubaliana kuendesha mafunzo ya pamoja ya mara kwa mara na kubadilishana mbinu sambamba na kuongeza ushirikiano jumla.

Amesema pia wamekubaliana kutoa mafunzo ya ugaidi pamoja na vifaa kwa lengo la kudhibiti zaidi vitendo hivyo.

Sirro amesema, licha ya kukubaliana kushirikiana na mabara mengine, lakini suala kubwa la kukabiliana na uhalifu na kupambana nalo linaanza na familia.

Museveni ampinga waziri wake wa utalii

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amepinga pendekezo la Waziri wa Utalii nchini humo, Godfrey Kiwanda la kuwatumia wanawake wenye maumbo makubwa kama kivutio cha watalii.

Amesema pendekezo hilo halijapitishwa na baraza la mawaziri na hawezi kuruhusu wanawake kuonesha miili yao kwa watalii.

Siku za hivi karibuni, Waziri wa Utalii nchini humo alipendekeza kuwe na onyesho la wanawake wenye maumbo makubwa ili kuvutia wageni zaidi wanaoitembelea nchi hiyo.

"Kwa nini hatutumii watu hawa kama mkakati wa kukuza sekta yetu ya utalii nchini Uganda?" Tovuti ya habari ya Uganda ya Daily Monitor ilimnukuu Kiwanda wakati wa uzinduzi wa ukurasa wa pamoja, Miss Curvy Uganda, jijini Kampala.

Kauli hiyo haikupokelewa vyema nchini humo hususan katika mitandao ya kijamii  sambamba na kupingwa na wanaharakati walioiita kauli hiyo kama "udhalilishaji".

Mkapa aamua kupumzika kutatua mgogoro wa Burundi

Rais Mstaafu wa awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ameachia ngazi nafasi ya kuendelea kuwa msuluhishi katika mazungumzo ya kutatua mzozo wa kisiasa nchini Burundi, msemaji wake ameieleza BBC.

Mgogoro huo wa kisiasa ulipamba moto mwaka 2015 baada ya Rais wa sasa Pierre Nkurunziza kujiongeza muhula wa tatu ulioleta sintofahamu nchini humo na kupingwa vikali na upinzani.

"Kipindi cha kusuluhisha kimefikia mwisho,’’alinukuliwa akisema Makocha Tembele.

Hata hivyo msemaji huyo amekanusha kuwepo kwa taarifa zinazodai kuwa Rais Mkapa amejiuzulu nafasi hiyo.

"Ni mwisho wa mamlaka yake," alisema, na kuongeza kuwa Mkapa ameshawasilisha ripoti yake ya mwisho wakati wa mkutano wa mwisho wa viongozi wakuu wa nchi za Afrika Mashariki uliofanyika mapema mwezi huu.

Tembele amesema kilichobaki ni kwa upande wake Rais wa Uganda, Yoweri Museveni kuendelea na awamu inayofuata ya usuluhishi ambayo inapaswa kufanyika kabla ya uchaguzi ujao unaotarajiwa kufanyika mwakani.

Hata hivyo mazungumzo hayo yalitokana na vurugu zilizotokea nchini humo na kuuawa watu takribani 1,000 yanaonekana kutofanikiwa kutokana na Serikali kwa mara kadhaa kugomea kutuma ujumbe katika vikao vinavyoitishwa na wasuluhishi hao.