Aliyetangazwa “kufariki” tangu Disemba ajifungua mtoto

|
Aliyetangazwa “kufariki” tangu Disemba ajifungua mtoto

Mwanamichezo wa kimataifa, Catarina Sequeira (26) aliyetangazwa na jopo la madaktari nchini Ureno kuwa ni mfu wa ubongo tangu Disemba mwaka jana, amejifungua mtoto wa kiume siku ya Alhamisi.

Mtoto huyo aliyepewa jina la Salvador, amezaliwa akiwa na uzito wa kilo 1.7kg baada ya kukua kwa wiki 32 tumboni mwa mama yake, na sasa yupo chini ya uangalizi katika moja ha hospitali ya watoto nchini humo.

Sequeira amezikwa Ijumaa, siku moja baada ya mtoto kutolewa tumboni mwake.

Mama mzazi wa Sequeira, Maria de Fátima Branco, ameiambia televisheni moja ya Ureno kuwa alimuaga binti yake Disemba 26, na uamuzi wa kumuacha mtoto huyo azaliwe ulifikiwa kutokana na shauku ya muda mrefu ya baba wa mtoto (Salvador), Bruno, kuhitaji mtoto.

Hii ni mara ya pili nchini Ureno kwa mtoto kuzaliwa kutoka kwa mama ambaye ni 'mfu wa ubongo'.

Sequeira ambaye alikuwa mwanariadha wa mbio za mitumbwi amekuwa akisumbuliwa na pumu toka utoto wake.

Shambulio lililochukua uhai wake lilimpata akiwa na mimba ya wiki 19, hali iliyomfanya kupoteza fahamu.

Siku chache akiwa chumba cha wagonjwa mahututi hali ilizidi kuwa mbaya na akatangazwa kuwa 'mfu wa ubongo' Disemba 26. Madaktari wakamuwekea mashine ya kusaidia kupumua ili mtoto tumboni aweze kuishi. Mashine hiyo iliwekwa kwa siku 56.

Chanzo: BBC

 

Health
Maoni