Askofu Nkwande ateuliwa kuwa Askofu Mkuu Jimbo la Mwanza

|
Askofu mteule wa Jimbo Katoliki Mwanza, Renatus Nkwande

Baba Mtakatifu, Francis amemteua Mhashamu Baba Askofu Renatus Nkwande kuwa Askofu Mkuu Jimbo la Mwanza, taarifa ya Baraza la Maaskofu Tanzania imesema.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa leo Februari 11 na balozi wa Papa nchini, Askofu Nkwande alikuwa akiliongoza Jimbo Katoliki la Bunda.

Askofu Kwande alizaliwa Novemba 12, 1965, Mantare mkoani Mwanza na kupata elimu yake ya Falsafa katika Seminari Kuu ya Kibosho kati ya mwaka 1987 hadi 1989 na kuendelea na elimu ya teolojia katika Seminari ya Mt. Karoli Lwanga, Segerea mwaka 1989 hadi 1994 na alipata daraja la upadri Julai 1995 katika Jimbo Kuu la Mwanza.

Amefanya kazi kama paroko msaidizi katika Parokia ya Magu, Mwanza 1995 hadi 1996 na mwaka 2005 alipata Shahada ya Uzamili katika Sheria za Kanisa huko Italia.

Aliteuliwa kuwa Askofu mwanzilishi wa Jimbo Jipya la Bunda mwaka 2010 na amekuwa askofu wa jimbo hilo hadi Februari 11, 2019 alipoteuliwa kuwa Askofu Mkuu Jimbo Kuu la Mwanza.

Tukio
Maoni