Barazani: Nafasi ya waziri kiongozi ilifutwa kwa mujibu wa sheria

|
Baraza la Wawakilishi Zanzibar

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema kufutwa kwa nafasi ya waziri kiongozi na mbadala wake kuwa makamu wa kwanza na wa pili wa rais kumefanyika kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar kupitia Marekebisho ya kumi ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010.

Hayo ameyasema Naibu waziri wa nchi, Ofisi ya makamu wa pili wa rais, Mihayo Juma Nanga alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na mwakilishi wa Jimbo la Fuoni Yussuf Khamisi aliyetaka kujua sababu za kufutwa  kwa cheo hicho licha ya Katiba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ya kutambua uwepo wa nafasi hiyo.

Naibu waziri wa nchi ofisi ya makamu  wa pili wa rais huyo amesema  marekebisho hayo yamefanywa kupitia matakwa ya wananchi  kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar na sheria zake  na kwamba hakuathiri shughuli za kiutendaji katika serikali zote mbili.

Katika hatua nyingine Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi imesema Zanzibar inapata mgao wa fedha kutokana na uvuvi wa bahari kuu kwa asilimia 20 huku Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikipata asilimia 30.

Akijibu swali lililoulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Mfenesisni Machano Othaman Saidi, Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Rashid Ali Juma amesema mgao huo hugawiwa katika sehemu tatu ambapo asilimia 50 inabaki ndani ya Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu.

Utawala
Maoni