Boeing yasitisha matumizi ya ndege zake zote 371

|
Miongoni mwa ndege aina ya Boeing 737 max 8 za Marekani zilizopigwa marufuku baada ya kutokea ajali ya Ndege ya Ethiopia na Lion Air

Kampuni ya utengenezaji ndege ya Boeing ya Marekani imesitisha matumizi ya ndege zote 371 aina ya ya Boeing 737 Max 8 baada ya wachunguzi kubaini ushahidi mpya katika eneo ambako ndege ya shirila la Ethiopia ilianguka na kuua watu wote.

Shirika linalosimamia usafiri wa anga Marekani FAA, limesema ushahidi mpya pamoja na data mpya za satelaiti zimechangia uamuzi huo wa kupiga marufuku kwa muda usafiri wa ndege hizo.

Maafisa wa FAA wanaochunguza mkasa huo katika eneo ambapo ajali ya shirika la ndege la Ethiopia ilipotokea, wanasema kuna mfanano wa namna ajali ya ndege ya Ethiopia ilivyotokea na ile ya shirika la Lion Air la Indonesia.

Awali FAA lilisisitiza ndege ya Boeing 737 Max 8 ni salama wakati mataifa mengine yakipiga marufuku usafiri wa ndege za aina hiyo.

Ajali ya Jumapili mjini Addis Ababa iliyosababisha vifo vya watu 157 ni ya pili kushuhudiwa ikihusisha ndege zenye chapa ya Max 8 katika miezi mitano baada ya ajali nyingine nchini Indonesia Oktoba mwaka jana iliyosababisha vifo vya watu 189 ikihusisha ndege ya kampuni ya Lion Air.

Usafiri
Maoni