Burundi yamnyoshea kidole Rwanda, yataka mkutano maalumu wa usuluhishi

|
Rais wa Burundi, Pierre Nkurunzinza aliyemwandikia barua mwenyekiti wa EAC, akiishutumu Rwanda kwa uasi

Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza amesema kuna mzozo wa wazi kati ya taifa lake na taifa jirani la Rwanda katika kinachoonekana kuwa kudorora zaidi kwa uhusiano baina ya mataifa hayo mawili.

Rwanda na Burundi zimekuwa na uhasama kwa muda sasa huku Burundi ikiituhumu Rwanda kwa kuhusika katika jaribio la kupindua Serikali yake mwaka 2015 ambalo lilishindwa.

Kwa mujibu wa BBC, Burundi imedai kwamba Rwanda iliwafadhili waliohusika na jaribio hilo na kwamba inatoa hifadhi kwao.

Hata hivyo Rwanda yenyewe mara kwa mara imekuwa ikikanusha tuhuma hizo.

Kwa mujibu wa vyonzo vya uhakika, Rais Pierre Nkurunziza amemwandikia barua Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Yoweri Museveni ambaye ni Rais wa Uganda akimtuhumu Rwanda kama adui ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

"Rwanda ndiyo nchi pekee katika ukanda huu ambaye ni mmoja wa wahusika wakuu katika kuvuruga uthabiti wa taifa langu na kwa hivyo siichukulii kama taifa mshirika, lakini kama adui wa nchi yangu," ilisema sehemu ya barua hiyo ambayo imeonesha kutiwa saini na Nkurunziza Desemba 4.

Kiongozi huyo ametaka uitishwe Mkutano maalum wa EAC kwaajili ya kujadili mzozo huo kati ya Rwanda na Burundi.

Viongozi wa mataifa ya jumuiya hiyo ambayo kwa sasa inajumuisha nchi za Burundi, Rwanda, Uganda, Kenya, Tanzania na Sudan Kusini wamepanga kukutana Desemba 27 baada ya kushindwa kukutana mwishoni mwa juma lililopita kufuata Burundi kutoshiriki na kusababisha akidi kutotimia.

Utawala
Maoni