CCM yajipanga kufufua vyuo vyake vya mafunzo ya uongozi

|
Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, Dkt. Bashiru Ally

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimejipambanua kufufua vyuo vya mafunzo ya uongozi kwa vijana kimojawapo kikiwa ni Chuo cha Ihemi ambacho kilikuwa kikihusika na utoaji wa mafunzo ya itikadi na uongozi na kuimarisha jumuiya za chama

Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara Dkt. Bashiru Ally ameyasema hayo mkoani Iringa katika  ziara ya siku moja ya kikazi na kuzitaka Jumuiya zote kushirikiana na vijana  kuhakikisha chuo hicho cha Ihemi kinafufuliwa na kuanza kutoa mafunzo ya Itikadi na uongozi pamoja na ufundi stadi.

Chuo hicho cha Ihemi kinachotazamiwa kutoa mafunzo ya Itikadi na uongozi pia kitahusisha miradi mbalimbali kama ya ufugaji wa samaki, kilimo cha mazao na ufugaji wa ng’ombe huku Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Salim Abri ASAS akatangaza neema ya kuwasaidia cherehani za kisasa  pamoja na ng’ombe wawili kama kianzio.

Katibu mkuu amemaliza ziara yake kwa kutembelea maeneo ya ufugaji, maeneo ya kilimo, madarasa ya ufundi stadi, pamoja na kuzuru majengo yote yaliyopo eneo la Ihemi ambayo yapo chini ya Umoja wa Vijana na kuwataka kuhakikisha maeneo hayo wanayakatia hati ili wayamiliki kihalali na kuepuka migogoro ya ardhi.

Siasa
Maoni