CCM yatangaza kuzoa kata zote 47 katika uchaguzi mdogo

|
Katibu wa Itifaki na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza kunyakua kata zote 47 katika Uchaguzi mdogo uliofanyika Disemba 2 ambapo kwa mujibu wa matokeo ya jumla, CCM ilipita bila kupingwa katika kata 41 huku sita zikinyakuliwa kwa ushindi wa kishindo baada ya kufanyika kwa uchaguzi mdogo.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Katibu wa Itifaki na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amesema, CCM inawashukuru Watanzania na wanaCCM kwa kuendelea kukiamini chama hicho na kwamba watahakikisha wanaendelea kushirikiana na wananchi wote katika kuwapelekea maendeleo katika maeneo yao.

“CCM imeendelea kuongoza, inajivunia umakini mzuri wa kufuata Taratibu, Kanuni na Sheria za Nchi yetu, Sera nzuri, ahadi zinazotekeleka na siasa safi na uongozi bora.”

Wakati huo huo, Katibu huyo wa Uenezi, ametangaza kufanyika kwa vikao vya Chama kati ya Disemba 17 -18 jijini Dar es Salaam, ambapo kwa mujibu wa taarifa hiyo Polepole amesema, Disemba 17 kitafanyika kikao cha Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa na Disemba 18 kitaketi kikao cha Halmashauri kuu ya Taifa.

Katika hatua nyingine kupitia taarifa hiyo, Polepole ametolea ufafanuzi wa suala la Katibu mkuu wa CCM, Bashiru Ally kumwita mwanachama wa CCM, Benard Membe na kusema utaratibu huo ni wa kawaida ndani ya chama katika kuendelea kuimarisha Umoja na mshikamano wa wanaCCM.

Amewataka wanaCCM na wananchi kwa ujumla kupuuza taarifa zinazozagaa katika mitandao ya kijamii na baadhi ya magazeti na kusema yanayoendelea kwenye mitandao hiyo baadhi ni uzushi, uchonganishi, fitini na uvumi.

Kupitia taarifa hiyo Polepole amewataka Wana CCM na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuwa na Umoja, Mshikamano na Upendo zaidi katika kipindi hiki cha Mageuzi makubwa ya kiuchumi na ya kimaendeleo kwa watanzania wote.

Siasa
Maoni