CENI wamtangaza Tshisekedi, Rais mteule DR Congo

|
Felix Tshisekedi, mgombea wa upinzani aliyeshinda upinzani

Tume Huru ya Uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (CENI) imemtangaza mgombea wa upinzani, Felix Tshisekedi kuwa mshindi wa uchaguzi wa Urais nchini humo ambao matokeo yake yamesubiriwa kwa muda mrefu tangu uchaguzi ufanyike Disemba 30,  mwaka jan.

Ushindi wa Rais Mteule Tshisekedi unaifanya nchi hiyo kwa mara ya kwanza kushuhudia uongozi wa juu ukikabidhiana madaraka kwa njia ya Amani.

Kwa matokeo hayo yaliyosubiriwa kwa karibu wiki mbili tangu uchaguzi huo ufanyike, yamehitimisha hofu na mashaka sanjari na kauli za kuionya Tume ya Uchaguzi kutoka ndani na nje ya nchi zilitolewa zikiitaka tume hiyo kutochezea matokeo ya uchaguzi huo.

Mkuu wa Tume ya Uchaguzi CENI, Corneille Nangaa alitangaza matokeo hayo mbele ya waandishi wa habari usiku wa kuamkia leo.

"Kwa kupata kura halali 7,051,013, sawa na asilimia 38.57 ya kura zilizopigwa, Felix Tshisekedi ametangazwa kuwa rais mteule wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo."

Shangwe na vifijo vilitawala katika ofisi za tume, wakati matokeo hayo ya kihistoria yalipotangazwa huku leo katika mitaa ya Kinshasa, jiji hilo limekuwa kimya. Baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Ufaransa imesema matokeo hayo hayashabihiani na yale yaliyokusanywa na waangalizi wa Kanisa Katoliki.

DRC imekuwa katika mgogoro wa kumpata mrithi wa Rais Joseph Kabila ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 18, ambaye mwaka jana alisema angeachia madaraka.

Mgombea ambaye alimuunga mkono kuwa mrithi wake ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Ramazani Shadary, ameshika nafasi ya tatu katika matokeo ya uchaguzi huo.

Mgombea mwingine mkubwa wa upinzani, mtendaji mkuu wa zamani wa mafuta, Martin Fayulu ambaye alionekana kuwa chaguo la wengi katika kura za maoni kabla ya uchaguzi, ameshika nafasi ya pili.

Kwa mujibu wa ratiba ya awali iliyotolewa na CENI, matokeo kamili yanatarajiwa kutolewa Januari 15 na rais mteule ataapishwa siku tatu baadaye.

Matokeo hayo yanaweza kupingwa katika Mahakama ya Kikatiba.

uchaguzi
Maoni