CHADEMA waipinga Sheria mpya ya mifuko ya Hifadhi ya Jamii

|
Waziri Kivuli wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Ajira ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bunda, Ester Bulaya

Waziri Kivuli wa Sera Bunge Kazi, Vijana na Ajira ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bunda, Ester Bulaya  amewataka wafanyakazi nchini kuungana na kuifungulia kesi serikali huku akikosoa juu ya Sheria mpya ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2017 ambayo iliwasilishwa bungeni hivi karibuni na kujadiliwa na wabunge.

Mbunge huyo amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kusema, sheria iliyojadiliwa na Bunge inaenda kinyume na takwa la katiba sanjari na suala la nyongeza ya mshahara kwa mfanyakazi.

Mbunge huyo amesema aliamua kukaa kimya katika kipindi cha miaka mitatu ili kujua ni kwa jinsi gani serikali ya awamu ya tano inafanya kazi katika wizara ambayo yeye kama Waziri Kivuli anaihudumia.

Esther amesema, CHADEMA imejipanga endapo itachukua nchi kuwawezesha wafanyakazi kuwa na mazingira bora ya kazi kwa mujibu wa sera yao ambayo wameizindua hivi karibuni baada ya kubezwa kwa siku nyingi.

”Sisi katika sera yetu hii ambayo awali walisema hatuna sera, tukajifungia na kuitengeneza imeweka wazi namna tutavyowawezesha wafanyakazi, CCM hawana Sera wanayoitumia ni ya Serikali” alisema Ester Bulaya.

Amedai kuwa , dhamira ya kuunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii ilikuwa ni janja ya serikali kukwepa madeni inayodaiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii ambayo kwa sasa inafikia trilioni 8 kwa sababu waliwekeza kwenye miradi isiyokua na tija,” ameongeza.

Siasa
Maoni