Diamond Platnumz kuwapa vicheko wakazi wa Tandale

|
Mwanamuziki Diamond Platinum kesho kuwaambia asante Tandale

Katika wiki ya kusheherekea kuzaliwa kwake, Mwanamuziki maarufu, Nasib Abdul almaarufu Diamond Platnumz, Kesho Ijumaa Oktoba 5, anatarajiwa kuwafurahisha wakazi wa maeneo aliyokulia huko Tandale katika Uwanja wa TANDALE MAGUNIANI kwa kutoa misaada mbalimbali ya kuwainua kiuchumi wamama, vijana na wakazi wa maeneo hayo kwa ujumla.

Kupitia Mtandao wake wa Instagram, Diamond amesema, kesho atadhimisha siku yake hiyo kwa kuwapatia wakazi 1000 kadi za Bima za Afya ambazo zitawawezesha kutibiwa bure mwaka mzima.

Aidha katika kuwainua vijana wenzake, Diamond amepanga kuwapatia vijana wapatao 20 pikipiki maarufu Bodaboda zitazowasaidia kujiajiri na kuwainua kiuchumi sanjari na kina mama Lishe 100 watakaonufaika na msaada wa mtaji wa kuanzia shilingi 100,000 – 200,000.

“Katika siku hii nitajumuika pamoja na watandale wenzangu.... siku hio ambayo nimeipa jina la "Thank you Tandale" yani (Asante Tandale) itaambatana na vitu mbalimbali,” ilisema sehemu ya ujumbe wake katika mtandao wa Instagram.

Mbali na hayo mwanamuziki huyo nyota anataraji pia kukarabati shule za msingi zilizopo Tandale pamoja na kuweka matanki yatayosaidia kuhifadhi maji ili yakikatika wanafunzi na walimu waweze kupata hudumu hiyo muhimu kupitia tanki hizo.

Amesema katika siku hiyo kesho, ataambatana pia na wageni mbalimbali waalikwa wa kutoka serikalini sambamba na wale wa kwenye taasisi na kampuni mbalimbali pamoja na watu maarufu watakaosaidia kunogesha siku hiyo huko Tandale kwa lengo la kuwaoneshana vijana wa Tandale njia bora ya kufikia mafanikio. 

Muziki
Maoni