Dkt. Msonde atoa onyo kwa wadanganyifu wa mitihani ya Taifa

|
Katibu mtendaji mkuu wa Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania (NECTA), Dkt. Charles Msonde

Katibu mtendaji wa Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania (NECTA), Dkt. Charles Msonde ametoa onyo kwa shule zote na wanafunzi wote wa Kidato Cha Sita kutojihusisha na udanganyifu katika mtihani wa taifa unaotarajia kufanyika Mei 6, mwaka huu.

Katibu mkuu ameyasema hayo alipowatembelea wanafunzi zaidi ya 1000 wa kidato cha Sita mkoani Simiyu waliopo kwenye kambi ya kitaaluma katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa.

Akizungumza katika ziara yake hiyo, Dkt. Msonde ameupongeza Mkoa wa Simiyu kwa ubunifu uliofanya wa kuwakutanisha wanafunzi pamoja hali ambayo amesema inawawezesha kukabiliana na changamoto ya uhaba wa walimu hususani kwa masomo ya sayansi kwani kwa umoja huo walimu wachache waliopo wanaweza kuwafundisha wanafunzi wote.

Akitoa taarifa za kambi hiyo, Afisa Elimu Mkoa wa Simiyu, Ernest Hinju amesema Mkoa umeshuhudia mafanikio ya wanafunzi kukaa kambini kwa muda mfupi ambapo katika matokeo ya kitaifa ya kidato Cha Sita mwaka 2017, Mkoa ulishika nafasi ya mwisho na baada ya kuweka kambi za kitaaluma 2018 Mkoa ulipanda hadi nafasi ya 10.

Wanafunzi waliopo kambini kwa zaidi ya wiki tatu sasa wamesema wamejifunza mengi na kupata utayari wa kuukabili mtihani wa mwisho ifikapo Mei 6 huku wakiahidi kuupandisha Mkoa hadi nafasi ya tatu Bora kitaifa.

Elimu
Maoni