Dkt. Shein atoa msamaha kwa wafungwa 12

|
Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Mohamed Shein

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein ametoa msamaha kwa wafungwa 12 ambao wanatambulika kama wanafunzi waliokuwa wanatumikia vyuo vya Mafunzo vya Unguja na Pemba ikiwa ni sehemu ya shamra shamra za maadhimisho ya miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt. Abdulhamid Yahya Mzee imeeleza kuwa kwa mamlaka aliyopewa chini ya kifungu cha 59 cha Katiba ya Zanzibar 1984, Rais Dkt. Shein ameamuru kuwa kifungo kilichobaki cha wanafunzi walionufaika na msamaha huo, ambao bado wanaendelea kutumikia katika vyuo vya Mafunzo vya Unguja na Pemba kimefutwa na hivyo wapo huru kuanzia leo.

Walionufaika na msamaha huo kwa Unguja ni Mushtaki Mustafa Hashim, Ramadhan Abubakar Jabu, Bakari Khamis Juma, Maulid Kheir Suleiman, Othman Ramadhan Shija, Faiz Juma Faiz na Ali Haji Ali.

Wengine walionufaika na msamaha huo kwa upande wa Pemba ni Suleiman Ali Suleiman, Ali Omar Ali, Ibrahim Mbarouk Omar, Mohamed Othman Ali na Mbarouk Ali Mbarouk.

Msamaha huo ambao hutolewa kila mwaka katika kipindi cha Sherehe za Mapinduzi Matukufu, huwahusisha wanafunzi ambao ni wazee sana, wenye maradhi sugu au wenye makosa madogo ambao wamebakiza muda mfupi wa kutumikia chuoni, wanaoonesha nidhamu nzuri chuoni na kujutia makosa yao.

Kwa kawaida Wanafunzi wa Chuo cha Mafunzo, wenye makosa kama vile kuua kwa makusudi, wizi wa kutumia nguvu, wizi wa mali ya Umma, makosa ya kudhalilisha wanawake na watoto, makosa ya dawa za kulevya na wenye makosa mengi ya zamani huwa hawapewi msamaha.

Msahama huo ni sehemu ya shamra shamra za miaka 55 ya mapinduzi ya Zanzibar tangu kuasisiwa kwake.

Utawala
Maoni