Edward Lowassa arejea CCM, apokelewa na JPM

|
Edward Lowassa, akiwa pamoja na viongozi wa CCM mara baada ya kutangaza kurudi katika chama hicho Lumumba jijini Dar es Salaam

Waziri mkuu mstaafu, Edward Lowasa ametangaza kurudi katika Chama chake cha Mapinduzi (CCM) akitokea CHADEMA. Lowassa aliihama CCM na kujiunga na CHADEMA mwaka 2015 wakati wa kinyang'anyiro cha urais ambapo alipeperusha bendera ya CHADEMA akichuana na Rais John Mapinduzi.

Akizungumza mara baada ya kumpokea kiongozi huyo ambaye wakati wa kuhama CCM alitikisa nchi, Mwenyekiti wa CCM Magufuli amesema, Lowassa ameamua kurudi nyumbani yaani CCM baada ya kujitafakari kwa muda namna alivyokitumikia chama hicho tangu wakati wa vijana wa TANU, Ndugu zangu kama alivyozungumza Lowassa ametumia maneno mafupi amerudi nyumbani na nyumbani ni hapa CCM, ndiyo maana amesimama kwenye jengo la Makao Makuu Ofisi ndogo ya CCM.” 

Akizungumza katika Ofisi  ndogo za CCM zilizopo Mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam, Lowassa hakuwa na maneno mengi ya kueleza zaidi ya kuwaambia Watanzania kuwa ameamua kurudi nyumbani (CCM).

"Nimetafakari na sasa nimeamua kurudi nyumbani CCM ambako sehemu kubwa ya maisha yangu nimekuwa huko,"amesema Lowassa huku mamia ya wananchi wakiwamo wanachama na wapenzi wa CCM walikuwa wanamshangilia.

Wakati Lowassa anatangaza kurejea CCM alikuwa amesikindikizwa na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Igunga ambaye pia aliwahi kuwa Mtunza wa fedha wa CCM, Rostam Aziz.

Akizungumza baada ya Lowassa kurudi CCM, Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli amesema wamempokea Lowassa na katika kuthibitisha hilo waliona ni vema uamuzi wake akautangazia Ofisi za CCM Lumumba kama sehemu ya uthibitisho.

"Kama ambavyo amezungumza kwa kifupi mwenyewe Mzee Lowassa kwamba amerudi nyumbani ambako ni huku CCM, tumempokea. Amekuja kutangazia hapa Lumumba kama sehemu ya kutoa shuhuda.

"Kwa upande wetu tumekaa, tumetafakari na kujiridhisha Lowassa amekaa kwenye Chama kwa muda mrefu na kwa bahati mbaya zilizojitokeza aliamua kwenda upinanzani. Tumemsikiliza mawazo yake kwamba amekaaa kwenye Chama Cha Mapinduzi sehemu kubwa ya maisha yake na kwamba kutokana na sababu ambazo amezieleza aliamua kwenda upinzani na leo hii amerudi nyumbani,"amesema Rais Magufuli.

Hata hivyo kabla ya Rais Magufuli kuzungumza aliamua kuwatania watu waliokuwa wamejitokeza Lumumba na kuwaambia imekuaje wako hapo au wanamaono na hivyo walijua kitakachotokea.

Wakati huo huo Katibu Mkuu wa CCM Dk.Bashiru Ally amesema Lowassa amefikia uamuzi wa busara kwa kurudi nyumbani kwa ajili ya kushirikiana katika kuleta maendeleo ya wananchi wote.

"Amerudi nyumbani, kwa hiyo tunaanza kazi ya kujenga Taifa letu na kujenga utu wetu, Lowassa ni kiongozi ambaye ametoa mchango mkubwa katika nchi yetu. Kwa niaba ya Mwenyekiti wa Chama chetu tumepanga kumpokea na yupo tayari kushirikiana nasi kuwatumikia wananchi,"amesema Dk.Bashiru.

Siasa
Maoni