'Endeleeni kuuheshimu utamaduni wetu'

|
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua vyakula vya utamaduni wa watu wa Lindi katika tamasha la makabila ya huko

Waziri mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Watanzania waendelee kuuheshimu na kuuendeleza utamaduni ambao ndiyo urithi wao ili kulifanya Taifa liendelee kuwa hai.

Amesema suala la kuuenzi utamaduni ni jambo zuri ambalo linatoa fursa kwa watu wengine hususan wa mataifa ya nje kuja kujifunza historia ya Watanzania na maisha yao.

Waziri mkuu aliyasema yao jana jioni Ijumaa, Oktoba 26, alipotembelea shughuli za tamasha la utamaduni wa Mtanzania kwa jamii ya watu wa Lindi.

Katika tamasha hilo linalofanyika kwenye Kijiji cha Makumbusho jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwataka Watanzania kuendelea kuupenda utamaduni wao.

“Nimefurahi kuona nyumba zikiwa na zana mbalimbali za kitamaduni ambazo zilikuwa zikitumiwa na wazee wetu pamoja na namba ya utayarishaji wa vyakula vyetu vya asili.”

“Sikutarajia kuona haya ninayoyaona, nawashukuru wote walioshiriki katika kaandaa tamasha hilo pamoja na uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Kijiji cha Makumbusho.”

Waziri Mkuu alisema tamasha hilo ambalo limewakutanisha Wanalindi kutoka katika wilaya mbalimbali linatoa fursa ya wao pia kujadili maendeleo ya mkoa wao na Taifa kwa jumla.

Kadhalika, Waziri Mkuu aliwaomba wananchi wengi wajitokeze kwa wingi kwenda katika Kijiji cha Makumbusho kwaajili ya kujifunza historia ya Mkoa wa Lindi pamoja na fursa zilizoko.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi alisema mkoa umetumia tamasha hilo kutoa ujumbe kwa umma kuhusu vivutio mbalimbali walivyonavyo pamoja na fursa za uwekezaji.

Tamasha
Maoni