Ivory Coast wakubali kuandaa AFCON ya mwaka 2023

|
Rais wa CAF Ahmad Ahmad (kushoto) baada ya mazungumzo na Rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara.

Shirikisho la soka barani Afrika CAF limethibitisha kuwa Ivory Coast imeridhia kuwa mwenyeji wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2023.

Uamuzi huo wa Ivory Coast unahalalisha uwenyeji wa Cameroon fainali za mwaka 2021 baada ya kupokonywa zile za mwaka huu ambazo rasmi zitafanyika nchini Misri.

Kikao baina ya Rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara na Rais wa CAF Ahmad Ahmad, ndicho kilichomaliza mgogoro wa awali ambao ulifika hadi mahakama ya usuluhishi wa masuala ya michezo (CAS) kupinga kupokwa haki ya kuwa wandaaji wa fainali za mwaka 2021 na kupewa za mwaka 2023.

“Namshukuru Rais kwa ushirikiano alioutoa na kukubali kuiachia Cameroon michuano ya AFCON ya mwaka 2021 ambao tayari asilimia 80 ya maandalizi imekwishafanyika, huku wao Ivory Coast wakikubali kuandaa fainali za mwaka 2023, na Guinea wataandaa fainali za mwaka 2025”, amesema Ahmad.

Rais huyo wa CAF ameongeza kuwa katika fainali za mwaka 2025, Guinea wenyewe wana hiari ya kuamua kama watahitaji taifa lingine la kushirikiana nalo au la ingawa wao CAF wanaona ni vyema fainali hizo zikaandaliwa na mataifa mawili.

Mashindano ya AFCON kwa mwaka huu wa 2019 yatakuwa ya kwanza kushirikisha mataifa 24 kutoka 16 ya awali.

CAF
Maoni