Jaribio la mapinduzi lagonga mwamba Gabon

|
Kiongozi wa jaribio la mapinduzi nchini Gabon akitangaza kutokea kwa mapinduzi nchini humo kabla ya jaribio hilo kudhibitiwa na yeye pamoja wenzake watatu kukamatwa.

Wanajeshi wawili wameripotiwa kuuawa nchini Gabon siku ya Jumatatu kufuatia jaribio la kumpindua rais Ali Bongo ambaye anapatiwa matibabu nchini Morocco.

Askari wa tano anayedaiwa kuwa kiongozi wa jaribio hilo amekamatwa, ofisi ya rais imethibitisha.

Taarifa ya mapema leo ilisema wanajeshi wanne kati ya wanajeshi watano walikuwa wamekamatwa kwa kujaribu kufanya mapinduzi nchini Gabon.

Bado haijafahamika ilikuwaje hadi wanajeshi hao wawili kuuawa. Kiongozi wa uasi huo alikamatwa akiwa amejificha kwenye nyumba zilizopo jirani na kituo cha redio cha taifa alikotangaza kufanyika kwa mapinduzi hayo.

Msemaji wa serikali ya Gabon aliviambia vyombo vya habari vya Reuters na RFI kuwa jaribio hilo lilizimwa ndani ya muda mfupi.

“Serikali iko sawa na taasisi zote zinaendelea na shughuli zake,” Guy-Bertrand Mapangou alikiambia kituo cha France24.

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, (AU) Moussa Faki Mahamat, alitumia mtandao wa Twitter kulaani tukio hilo na kusema jaribio la mapinduzi nchini Gabon linalaaniwa vikali.

Na kuongeza kuwa AU haiwezi kuvumilia mabadiliko ya uongozi wa serikali usiofuata katiba.

Maisha
Maoni