Jimbo la Joshua Nasari latangazwa kuwa wazi

|
Joshua Nasari ambaye barua (kushoto) kwake ikiutangazia Umma kwamba amevuliwa rasmi ubunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Arusha

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungana wa Tanzania, Job Ndugai amemuandika barua, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Semistocles Kaijage kuwa Jimbo la Arumeru Mashariki kwa sasa liko wazi kufuatia, Mbunge wake Joshua Nasari ( CHADEMA) kushindwa kuhudhuria mikutano mitatu mfululizo na hivyo kupoteza sifa za kuendelea kuwa mbunge.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Spika Ndugai amesema, Mbunge Nasari hajahudhuria vikao hivyo vitatu mfululizo kikiwemo cha Mkutano wa kumi na kumi na mbili wa tarehe 4 -14 Septemba 2018 na mkutano wa kumi na tatu wa tarehe 6- 16 Novemba mwaka 2018.

Mkutano mwingine ambao Nasari anadaiwa hajahudhuria ni wa kumi nne wa tarehe 29 Januari  hadi Februari 9, 2019.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uamuzi huo wa spika umezingatia masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 71 (1) C ambayo inaeleza kuwa, “mbunge atakoma kuwa mbunge na ataacha kiti chake katika Bunge ikiwa atakosa kuhudhuria vikao vya mikutano vya Bunge mfulululizo bila ya ruhusa ya spika.”

Kanuni hiyo pia ikisaidiwa na ile ya 146 (1) na (2)  za Kanuni za Kudumu za Bunge toleo la Januari 2016. Kutokana na taarifa hiyo Tume ya Uchaguzi inaweza kuendelea na mchakato wa kupata Mbunge wa kujaza nafasi hiyo iliyo wazi katika Jimbo hilo la Arumeru Mashariki.  

Siasa
Maoni