JPM azitaka wizara husika kutatua kasoro za tozo zilizolalamikiwa

|
Rais John Magufuli akiendesha majadiliano na makundi ya wachimbaji wadogo wadogo

Rais John Magufuli amewaagiza viongozi wa Wizara ya Madini na Wizara ya Fedha na Mpango kujadiliana na kukubaliana na wadau wa madini kuhusu utaratibu mzuri utakaowezesha kuongezeka kwa mapato yatokanayo na madini yote yanayozalishwa nchini ikiwemo kupendekeza viwango vya tozo za kodi na ushuru vitakavyowavutia wadau kulipa tozo hizo badala ya kukwepa.

Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo Januari, 22 katika mkutano uliofanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam baada ya kupokea maoni ya wachimbaji wadogo, wafanyabiashara na wadau wengine wa sekta ya madini wanaokutana kwa siku mbili kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yahusuyo madini.

Katika maoni yao wadau hao wa madini wamemueleza, Rais Magufuli kuwa tozo kubwa na nyingi zilizowekwa katika madini hususan dhahabu zimesababisha wachimbaji wadogo na kati na wafanyabiashara wengi kukwepa kuuza madini yao katika utaratibu rasmi, hali inayosababisha zaidi ya asilimia 90 ya dhahabu inayozalishwa nchini kutoroshwa na hivyo kusababisha Serikali kukosa mapato.

Wamezitaja tozo hizo kuwa ni Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) inayotozwa kwa asilimia 18, Kodi ya zuio ya asilimia tano (5), kodi ya ukaguzi ya asilimia moja (1), ushuru wa huduma wa asilimia 0.3, mrahaba wa asilimia sita (6) na hivyo kufanya jumla ya tozo kuwa asilimia 30.3, na baadaye wanatozwa kodi ya kampuni kwa mwaka ambayo ni asilimia 30 ya faida.

Aidha, wadau hao wameomba wataalamu na viongozi wa madini wawe karibu na wachimbaji ili kujua uhalisia wa uchimbaji na biashara yake, kutafuta suluhisho la madini yaliyozuiliwa kusafirishwa nje ya nchi kutokana na kukosekana kwa mitambo ya kuchakatia, kupunguza gharama za leseni, kuanzisha vituo vya masoko ya madini, kupata bei elekezi ya madini ya viwanda na ujenzi na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kununua dhahabu.

Rais Magufuli amesema Serikali itakuwa tayari kufanyia kazi mapendekezo ya wadau hao yenye lengo la kuongeza ukusanyaji wa mapato ikiwemo kupeleka Bungeni marekebisho ya sheria zinazohusu tozo za madini ili nchi iweze kunufaika na rasilimali hiyo, tofauti na sasa ambapo utoroshaji wa madini, ukwepaji wa kodi na wizi vinasababisha madini ya Tanzania kuzinufaisha nchi nyingine.

Amemtaka Waziri wa Madini, Doto Biteko kuhakikisha anachukua hatua za haraka za kufanya mabadiliko katika maeneo yote yaliyoonesha udhaifu ndani ya wizara hiyo ikiwemo kuwaondoa viongozi na wataalamu ambao wamekuwa chanzo cha upotevu wa mapato ya Serikali, kutafuta wawekezaji watakaojenga viwanda vya kuchenjua na kuchakata madini na kuanzisha vituo vya kuuzia madini.

Rais Magufuli ametoa siku 30 kwa Waziri Biteko kuhakikisha ukuta wa kuzunguka madini ya Tanzanite wa Mererani unawekewa kamera za ulinzi na vifaa vya ukaguzi kwa wanaoingia na kutoka katika eneo hilo, pamoja na kuondoa sharti linalowataka vijana wenye ajira ndiyo waruhusiwe kuingia, hali iliyosababisha kuwepo malalamiko kuwa linasababisha vijana wasio na ajira kuingia kwa kuruka ukuta na kuwepo uhaba wa wachimbaji migodini.

Pia amemuagiza Waziri Biteko kuhakikisha maeneo yote ya madini ambayo yanashikiliwa na watu bila kufanyiwa kazi yananyang’anywa ili wapewe wachimbaji ambao wapo tayari kuchimba madini, kwa kutoa kipaumbele kwa wachimbaji wadogo na wa kati ambao wametajwa kufikia Milioni Sita (6).

Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Madini, Doto Biteko, Waziri wa Fedha na Mipango, Philip Mpango, Baadhi ya Wakuu wa Mikoa, Makatibu Wakuu, viongozi wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Viongozi wa Dini na viongozi wa vyama vya siasa. 

Madini
Maoni