JPM atoa wito wa Afrika kushirikiana kudhibiti upotevu wa fedha

|
Rais John Magufuli alipompokea aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki

Rais John Magufuli amesema Afrika ina kila sababu ya kuamka na kushirikiana vilivyo kukabiliana na tatizo la upotevu wa fedha ikielezwa kwa mwaka hupoteza kati ya dola za Marekani Trilioni 1. 4 mpaka Trilioni 2. 5, ambapo Tanzania pekee imepoteza dola za Marekani Bilioni 19 katika miaka 40 iliyopita.

Ameyasema hayo leo, Novemba 28 Ikulu Dar es Salaam baada ya kukutana na Thabo Mbeki ambaye ni Mwenyekiti wa jopo la ngazi ya juu lililoundwa na Umoja wa Afrika (AU) kushughulikia tatizo la utoroshaji wa fedha.

Rais Magufuli amekuwa na ugeni wa Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki ambaye alifika nchini na kisha kujadiliana juu ya namna Tanzania inavyokabiliana na utoroshaji wa fedha katika maeneo mbalimbali ikiwemo kudhibiti rushwa na sekta ya madini.

Katika mazungumzo yao wamerejea Ripoti ya Taasisi ya Kimataifa ya Global Financial Intergrity ya mwaka 2014 kuhusu utoroshaji wa fedha za Afrika inayosema kwamba Afrika imepoteza Dola za Marekani Trilioni 95 kwa miaka 50 iliyopita hali iliyowashtua viongozi wa Bara hilo.

Kutokana na hilo,. Rais Magufuli amesema Tanzania ipo tayari kutoa ushirikiano wa kutosha kunusuru rasilimali za Afrika.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway, Nicolai Astrup ambaye amesema wataendelea kuunga mkono juhudi mbalimbali za maendeleo nchini wakiahidi kutoa shilingi Bilioni 127.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro, Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba na Balozi wa Norway nchini, Elisabeth Jacobsen.

Fedha
Maoni