JPM awataka Watanzania kusheherekea Uhuru huku wakitafakari walipotoka

|
Rais John Magufuli

Rais John Magufuli amewatakia kila la kheri Watanzania wote katika maandalizi ya kuelekea kuadhimisha miaka 57 ya Uhuru na kuwataka mwaka huu badala ya kusheherekea Siku hiyo, wapumzike na kuitumia siku hiyo kutafakari Uhuru walionao; mahali walipotoka, walipo sasa na wanakoelekea.

Rais Magufuli amesema hayo leo, Novemba 7 wakati akilihutupia Taifa Ikulu jijini Dar es Salaam na kuwashukuru sambamba na kuwapongeza wazee wa Taifa hili wote waliosaidia kuikomboa nchi ya Tanzania kupata Uhuru wakiongozwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Katika salamu zake hizo, Rais Magufuli amesema, takribani shilingi bilioni moja zilizotengwa kwa ajili ya sherehe hizo lakini ameonelewa kwa sasa zitumike kujenga Hospitali ya Uhuru katika Jiji la Dodoma na kuwaomba Watanzania wote kufanyakazi kwa bidi ili kutafakari Uhuru uliopo na jitihada zinazofanyika ili kujikomboa kiuchumi..

“Kama mnavyofahamu, ili kutekeleza mawazo ya waasisi wetu, Serikali imeamua kuhamishia rasmi Makao Makuu ya nchi yetu Jijini Dodoma. Hii imefanya mahitaji ya huduma za jamii, ikiwemo afya, kuongezeka. Hivyo, tumeamua kujenga Hospitali nyingine kubwa itakayosaidiana na Hospitali ya Benjamin Mkapa na Hospitali ya Mkoa.” Alisema Rais Magufuli.

Mbali na hilo, Rais Magufuli pia kwa mujibu wa Mamlaka aliyopewa kwenye Ibara ya 45 (1) (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametoa msamaha kwa wafungwa 4,477, ambapo kati yao wafungwa 1,176 watatoka siku ya Maadhimisho ya Uhuru.

Rais Magufuli amesema, msamaha huo utawahusu wafungwa ambao ni wagonjwa, wazee kuanzia miaka 70 na zaidi, wafungwa wa kike waliongia gerezani wakiwa wajawazito na waliongia na watoto wanaonyonya au wasionyonya pamoja na wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili.

Rais Magufuli amesema, msamaha huo hautawahusu wafungwa wanaotumikia baadhi ya adhabu, zikiwemo kunyongwa, kifungo cha maisha, biashara ya dawa za kulevya na binadamu, makosa ya unyang’anyi, kukutwa na viungo vya binadamu, makosa ya kupatikana na silaha, risasi, milipuko isivyo halali, makosa ya shambulio la aibu, kunajisi, kubaka, kulawiti, kuwapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na sekodari, uhujumu uchumi, rushwa, ubadhirifu, ujangili, waliowahi kupunguziwa kifungo kwa msamaha wa Rais, wanaotumikia kifungo chini ya Sheria ya Bodi ya Parole, wenye makosa ya kutoroka au kujaribu ama kusaidia kutoroka chini ya ulinzi halali, waliongia gerezani baada ya Disemba Mosi, 2018 au waliowahi kufungwa na kurudi tena gerezani pamoja na wenye makosa ya kinadhamu magerezani.

Rais Magufuli pia amesema Watanzania wanapaswa kusheherekea siku hiyo ya Uhuru na kutambua kuwa kama nchi bado ina safari ndefu ya kufika kule wengi wanakotamani kufika; ambako ni kujenga Tanzania iliyo imara zaidi, yenye amani na umoja.

Amesema licha ya changamoto nyingi kama nchi imepitia tangu kupatikana kwa Uhuru mwaka 1961 kutoka kwa Waingereza, anafarijika kuona mafanikio kadhaa yaliyofikiwa lakini pia anatamani kuona Tanzania yenye maendeleo ya kiuchumi na inayojitegemea, Tanzania ambayo huduma za kijamii zinapatikana kwa urahisi zaidi na yenye watu walioelimika na wenye kipato kizuri.

Utawala
Maoni