JPM: Nchi isyo na umeme wa uhakika kupata maendeleo ni ndoto

|
Rais John Magufuli akiwa na Balozi wa Sweden wakizundua mradi wa kusafirisha umeme kutoka Makambako hadi Songea

Rais Magufuli amesema, nchi isiyokuwa na umeme nafuu na wa uhakika na usiojitosheleza kupata maendeleo ni ndoto.

Rais Magufuli ameyasema hayo wakati akizungumza na umma wa wananchi wa mkoani Ruvuma alipokuwa akizundua mradi wa kusafirisha umeme kutoka Makambako hadi Songea wenye jumla ya kilovotts 220.

Akizungumzia umuhimu wa kuwepo kwa upatikanaji wa umeme wa kutosha na uhakika Rais Magufuli amesema idadi ya watu imekuwa ikiongezeka tangu uhuru huku hali ya umeme ikiwa haitoshelezi.

Amesema, Tanzania imeamua kuingia katika uchumi wa viwanda na ili kuwezesha hilo ni lazima umeme uwe wa uhakika ambao utasaidia uzalishaji bidhaa zitakazouzwa kwa bei nafuu sanjari na kuongeza ajira.

“ Huwezi kuwa na viwanda unategemea umeme wa dizeli, hivyo huwezi kushindana na viwanda vya nchi zinazoendelea ambazo umeme wao ni wa uhakika na viwanda vyao vitazalisha bidhaa na kuziuza kwa bei nafuu na hivyo sisi tutaendelea kuwa wazalishaji wa malighafi na kushindwa kuzalisha ajira.” Alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema, miradi inayoendelea kuzalisha umeme nchi hadi sasa imeshaokoa takribani shilingi bilioni 217 kutoka uzalishaji wa umeme wa kutumia mitambo na mafuta.

Akizungumzia athari za kukosekana kwa umeme wa uhakika, Rais Magufuli amesema tatizo hilo limepelekea nchi ya Tanzania kupoteza takribani hekta 400,000 kila mwaka kwaajili ya wananchi kutafuta mkaa na kuni sanajri na kuharibu mazingira.

Amesema mbali na hilo pia kwa mujibu wa Benki ya MAENDELEO YA AFRIKA imeitaja Tanzania kupoteza maisha ya watu takribani 600,000 kwa mwaka kutokana na ajali na maradhi mbalimbali yanayotokana na matumizi ya nishati mbadala kama kuni, mafuta na mengine.

Aidha Rais Magufuli amemtaka Balozi wa Sweden nchini kuwaeleza wadau wenzake wa maendeleo kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi inayolinda mazingira yake kwa kiwango cha juu.

"Tanzania inajali sana utunzaji wa ardhi na uhifadhi, hivyo tunapotumia sehemu ndogo kwa ajili ya matumizi ya umeme ili kuwakwamua wananchi wetu tunaomba mtuelewe, msituzuie bali mtuunge mkono." Alisema Rais Magufuli.

Aidha amesema, hakuna Taifa lisilopenda kuona watu wake wanajikwamua na ugumu wa maisha na kumtaka Balozi huyo wa Sweden ambaye nchi yake imechangia katika mradi huo kuendelea kuiunga mkono Tanzania kwani dhamira ya serikali ni kuona wananchi wanapunguziwa ukali wa maisha kwa kuwa na umeme wa kutosha na uhakika.

“Nimefurahi kumuona balozi wa Sweden hapa ili aone kuwa fedha zinazotolewa zinatumika ipasavyo hakuna rushwa kwani azma na dhamira ya serikali ni kuifanya nchi yetu kuwa na umeme wa kutosha na wa bei nafuu,”

Rais Magufuli amewataka pia TANESCO kuutunza mradi huo kwa kuwa ni MALI YA UMMA na kuwataka wananchi kutunza vyanzo vya maji na misitu na kuwataka kuacha tabia ya uvamizi wa mazingira na kukata miti hovyo.

"Niwaombe wananchi, msivamie maeneo na msiingie misitu. Unakuta yuko katikati ya pori halafu anasema tunaomba mtulindie mazao yetu wakati umewaingilia wanyama pori. Tuitunze misitu, msikate miti. Mkiharibu mazingira yatatuadhibu." alisema Rais Magufuli.

Nishati
Maoni