Kamati za Bunge zawaalika wadau kuwasilisha maoni yao

|
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Kamati za Kudumu za Bunge tatu (3) zinatarajiwa kupokea na kusikiliza maoni ya Wadau kuhusu Miswada  Mitano (5) ya Sheria ya huduma za maji na Usafi wa mazingira ya mwaka 2018, Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2018.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kitengo cha habari, Elimu kwa Umma na Mawasiliano, Ofisi ya Bunge, Kamati hizo zitakuwa zikifanya vikao vyake vya kupokea na kusikiliza maoni ya wadau katika Jengo jipya la Utawala, Bungeni Jijini Dodoma kuanzia saa 3:00 Asubuhi.

Ratiba ya vikao hivyo inatarajiwa kuanza Januari 16 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji itakayopokea na kusikiliza maoni ya wadau kuhusu Muswada wa Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa mazingira wa Mwaka 2018 katika chumba Namba 43  huku Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu itakutana na wadau wake kwa ajili ya kusikiliza na kupokea Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania wa Mwaka na Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini wa Mwaka 2018 katika ukumbi Namba 38.

Aidha kwa upande wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria itapokea na kusikiliza maoni ya wadau kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa Mwaka 2018 na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 4) wa Mwaka 2018 kwa siku mbili mfululizo kuanzia Januari 17 na 18 katika ukumbi Na. 9.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Januari 19 na 20 Kamati hiyo pia itapokea na kusikiliza maoni ya wawakilishi kutoka kila Chama cha Siasa kilichosajiliwa nchini kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa Mwaka 2018 

Kamati pia zinawaalika wadau kufika na kuwasilisha maoni yao kwa lengo la kusaidia katika uchambuzi wa miswada hiyo ambayo inapatikana katika Tovuti ya Bunge www.parliament.go.tz sanjari na kuyawasilisha kwa njia ya Posta au Baruapepe kwa anuani ifuatayo:-  

Katibu wa Bunge,

Ofisi ya Bunge,

S.L.P 941,

DODOMA.

Baruapepe: cna@bunge.go.tz

Bunge
Maoni