Kanye West ajivunia urafiki wake na Trump

|
Kanye West akikumbatiana na rafiki yake Rais Donald Trump huku akiwa amevaa kofia yake "Make America great again"

Mwanamuziki machachari wa muziki wa kufokafoka maarufu kama RAP Kanye West ameendelea kuthibitisha ‘mahaba’ yake kwa Rais wa sasa wa Marekani Donald Trump baada ya kudai kuwa kofia ya Trump yenye maneno ya “Make America great again” humpa nguvu kama superman.

Mwanamuziki huyo ambaye mara kwa mara ameshindwa kuficha hisia zake kuhusu kumpenda na kumkubali Rais Trump kwa muda mrefu amekuwa akiweka wazi hisia zake kupitia ukurasa wake wa Twitter na mahojiano mbalimbali.

Katika kila unalofanya wapo watakaokuunga mkono na wale watakaokupinga, hata hivyo Kanye West amekuwa akiwazodoa wale wanaomkosoa na kuwataka wamuache awe huru.

Kanye West alialikwa katika Ikulu ya Marekani kwaajili ya chakula cha mchana na kujadili masuala mbalimbali ikiwemo mageuzi katika magereza, ajira na masuala ya wamarekani weusi.

Katika mjadala huo unadaiwa ulijaa vioja vingi kutokana na ukweli kwamba Trump na Kanye wote ni wazungumzaji na hutumia zaidi mtandao kuweka wazi hisia zao.

Katika majadiliano hayo yaliyolenga siasa, mageuzi na uzalishaji, West alinukuliwa akisema "wamejaribu kunitisha, marafiki zangu kuhusu kuvaa hii kofia, lakini hii kofia inanipa nguvu".

Kanye alienda mbali zaidi na kusema kofia hiyo iliyoandikwa "Make America great again" maneno yanayowakilisha kauli mbiu ya utawala wa Donald Trump inamfanya ajionee fahari  na kuongeza kuwa Trump ametengeneza kofia shujaa kwa ajili yake.

Muziki
Maoni