Kauli ya mkuu wa majeshi Algeria yachochea maandamano

|
Mkuu wa Majeshi wa Algeria akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa nchi hiyo, Abdelaziz Bouteflika kabla ya kumtaka aachie ngazi

Kauli ya Mkuu wa Majeshi ya Algeria kumtaka Rais Abdelaziz Bouteflika kuachia ngazi imechochea maandamano zaidi ya wananchi na ya watu wa kada mbalimbali ambao kwa takribani mwezi mzima sasa wamekuwa mitaani wakimshikiza kiongozi huyo kukaa pembeni na kuwaachia nafasi watu wengine.

Tayari Chama Tawala cha FLN ambacho Rais Bouteflika anatokea kimemtaka kiongozi huyo aachie madaraka ikiwa ni mwendelezo wa shinikizo kama hilo lililotolewa na chama mshirika wake cha RND.

Jana Mkuu wa Majeshi ya Algeria, Jenerali Ahmed Gaed Salah alisema imefika wakati sasa Katiba ya nchi itumike kutangaza kuwa Rais Abdelaziz Bouteflika hafai kutawala tena jambo ambalo limeibua mitazamo mbalimbali kwa wananchi.

Mamia ya wanafunzi ambao ndiyo wamekuwa kichocheo kikubwa cha maandamano mjini Algiers, wameonekana tena mitaani wakiunga mkono msimamo wa mkuu huyo wa majeshi ya nchi hiyo ambaye pia ndiye Naibu waziri wa Ulinzi wa Algeria.

Maandamano hayo yanafanyika wakati ambapo WaAlgeria wanasubiri mchakato wa kibunge kuhusiana na Ibara ya 102 ya Katiba inayoelekeza kuwa Rais anapaswa kuondoka madarakani ama kwa kujiuzulu au kutangazwa hafai kutawala kutokana na ugonjwa, hoja ambayo ni sharti ipigiwe kura na Bunge.

Utawala
Maoni