Kesi ya kina Mbowe yaahirishwa tena Kisutu

|
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeahirisha kesi inayowakabili viongozi wa CHADEMA, hadi Disemba 21 kwaajili ya kutajwa wakati ikisubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufaa iliyokatwa na upande wa mashtaka kupinga usikilizwaji wa rufaa ya Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na Mbunge wa Ester Matiko.

Aidha Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Wilbard Mashauri ameridhia taarifa ya kutofika mahakama kwa Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche ambao wako nchini Burundi wakishiriki michuano ya mabunge ya Afrika Mashariki.

Hakimu mkazi huyo na upande wa mashtaka wamesema hawana pingamizi juu ya uwepo wa taarifa za uzuru huo kutokana na kupokea nakala za barua za ruhusa kutokana Bungeni.

Katika Kesi hiyo iliyotajwa leo  Disemba 6, Mbowe na viongozi wakuu wa Chadema hicho, wanakabiliwa na mashtaka 13 ya uchochezi, uasi na kuhamasisha wafuasi wao kutenda makosa pamoja kufanya mkusanyiko kinyume na Sheria za nchi.

Taarifa ya kutofika mahakamani hapo kwa Mbunge Mdee iliwasilishwa pia na mdhamini wake, Farws Robson aliyeieleza mahakama kuwa mbunge huyo hakuweza kufika kwa kuwa yuko Burundi kwa safari ya kibunge akishiriki michezo ya wabunge wanawake wa mabunge ya Afrika Mashariki.

Robson ameieleza mahakama kuwa Katibu wa Bunge alimwandikia barua Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu kuhusiana na safari ya Mdee na kwamba anatarajia kurejea nchini Desemba 20, 2018.

Akitoa uamuzi wa mahakama baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Wilbard Mashauri amesema kwa kuwa alipokea nakala ya barua ya Bunge ikimwombea ruhusa Mdee  amekubali aendelee na shughuli zake hizo, wakati kwa upande wa Heche amesema anamruhusu aendelee na ruhusa yake ya kumuuguza mkewe ambayo alishampatia.

Hata hivyo amewataka washtakiwa wote wawepo tarehe hiyo 21 kesi hiyo itakapotajwa.

Wanaoshtakiwa katika kesi hiyo ni pamoja na Mwenyekiti Freeman Mbowe, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Tarime vijijini, John Heche, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Vicent Mashinji; Naibu katibu wakuu wa Bara, John Mnyika  na Salum Mwalimu  wa Zanzibar pamoja na mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.

Wengine ni mweka hazina wa Baraza la Wanawake la chama hicho (Bawacha), Esther Matiko na Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo Februari 16, 2018 katika viwanja vya Buibui wilayani Kinondoni wakati wakihutubia katika mkutano wa hadhara wa kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Kinondoni.

Mahakamani
Maoni