KIA wajipanga kuzipokea ndege za mashirika makubwa duniani

|
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) (Maktaba)

Leo ni Maadhimisho ya Siku ya Anga Duniani ambapo mataifa mbalimbali ulimwenguni huungana kuadhimisha siku hii.

Kwa Tanzania siku hii imeadhimishwa kwa aina yake ambapo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) wafanyakazi wa sekta hiyo walikusanyika kwa pamoja na kuzungumza na wanahabari juu ya hatua za awali za mazungumzo na mashirika makubwa ya ndege duniani yanayotarajiwa kuanzisha safari zao katika uwanja huo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu mkurugenzi wa KIA, Mhandisi Martin Kinyamagoha amesema, hatua hiyo wanaamini huenda ikaongeza maradufu idadi ya watalii wanaofika nchini kutembelea vivutio kadhaa hususani vile vilivyoko katika ukanda wa kaskazini.

Amesema , kwa sasa Shirika la Ndege la Ethiopia hufanya safari zake kila siku katika uwanja huo pamoja na Shirika la Kiholanzi la KLM ambayo kwa pamoja huleta  takribani watalii 700 kwa siku.

 

Kampuni ya KADCO inayosimamia uendeshaji wa Uwanja wa KIA imesema zaidi ya euro milioni 37 zimetumika kukarabati uwanja huo kukidhi viwango vya  juu  vya huduma za anga na sasa tambo kubwa zinapigwa kuelekea kuvuta mashirika kama Emirates na South African Airways kuanzisha safari mpya katika uwanja huo.

Wakati huo huo katika kuadhimisha siku hiyo ya Anga duniani, Jijini Dar Es Salaam, Kaimu Mkrugenzi wa Mamlaka ya Anga nchini, Mbuttolwe Kabeta amesema wakati wakiadhimisha siku hiyo ya kimataifa nchini zoezi la ufungaji wa rada katika viwanja vya ndege linatarajiwa kukamilika mwezi Desemba 2019 ambapo kwa sasa rada inayotakiwa kufungwa mkoani Mwanza tayari imeshawasili.

Biashara
Maoni