Kitilya na wenzake wafutiwa mashtaka na kukamatwa tena

|
Aliyekuwa kamishna wa TRA, Harry Kitilya na wenzake waliokuwa watumishi wa Benki ya Stanbic, Shose Sinare na Sioi Solomon wakiwa katika Mahakama ya Mkazi Kisutujijini Dar es Salaam

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewafutia mashtaka aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Harry Kitillya, maofisa wawili wa Benki ya Stanbic, Shose Sinare na Sioi Solomon baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kueleza mahakama hiyo kuwa hana nia ya kuendelea na shauri lao na kisha kukamatwa tena na kusomewa mashtaka 58 ikiwemo 49 ya utakatishaji fedha.

Uamuzi huo umetolewa leo Januari 11, ambapo washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka nane yakiwemo ya kutakatisha fedha na kwamba wamefutiwa kesi hiyo chini ya Kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), Sura ya 20 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Kabla ya kukamatwa tena, Wakili Mkuu wa Serikali, Hashimu Ngole akisaidiana na wenzake Pendo Mangole na Patrick Mwida, alidai kuwa DPP hana nia ya kuendelea na shauri hilo dhidi ya washtakiwa.

"Taarifa hii ya kutokuendelea na shauri hili mbele ya mahakama yako, imeletwa chini kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), sura ya 20, iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002," amesema Ngole. Baada ya maelezo hayo,

Hakimu Salum Ally alisema kutokana na maombi hayo, mahakama hiyo imeifuta kesi hiyo hata hivyo watuhumiwa hao walikamatwa tena mara tu baada ya kuachiwa na kupelekwa tena mahabusu.

Katika kesi hiyo mpya namba 2 ya mwaka 2019, washtakiwa hao wameongezewa washtakiwa wengine wawili na kufanya idadi ya washtakiwa kuwa Watano ambao wamesomewa mashtaka 58 na mawakili wa serikali kwa njia ya kupokezana wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Hashimu Ngole mbele ya Hakimu Augustina Mmbando.

Miongoni mwa mashtaka hayo 58 ni matatu ya kughushi na kusababisha hasara kwa serikali, kutoa nyaraka za uongo, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kutoka nyara za uongo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na 49 ya  Utakatishaji Fedha

Katika kosa la utakatishaji fedha inadaiwa washtakiwa wote walilitenda Machi 18, 2013 na Januari 10, 2014 wakiwa jijini Dar es Salaam ambapo walitakatisha dola za Marekani 6,000,000 kwa kuzitoa fedha hizo kupitia njia ya benki kwa jina la Enterprises Growth Market Advisors (EGMA) katika Benki ya Stanbic Tanzania.

Pia katika kosa la kusababisha hasara kwa Serikali, wanadaiwa kwa pamoja walilitenda kosa hilo Mei 1, 2012 na Juni 1, 2015 wakiwa jijini Dar es Salaam walijipatia Dola za kimarekani Milioni 600, 000,000 kama ada ya mkopo uliochukuliwa na Serikali ya Tanzania kutoka katika asilimia 1.4 hadi 2.4 na kusababisha Serikali ipate hasara ya Dola Milioni 6,000,000.

Upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na

Baada ya kusomewa mashtaka hayo Kesi imeahirishwa hadi Januari 24, 2019 kwa ajili ya kutajwa ambapo  washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama haina mamlaka.  

Mbali na Kitilya washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa miss Tanzania (1996), Shose Sinare na Ofisa wa Benki ya Stanbic, Sioi Solomon huku washtakiwa wapya walioongezwa ni Kamishna wa Sera ya Uchambuzi wa Madeni Wizara ya Fedha, Bedason Shallanda na Msaidizi wake, Alfred Misana.

Mahakamani
Maoni