Test
Samaki mwenye sumu azua taharuki Japan

Mji mmoja nchini Japan umetoa tahadhari na kutangaza hali ya hatari kwa kuzuia watu kula samaki anayejulikana kama Fugu baada ya samaki huyo mwenye sumu kali kuuzwa kimakosa.

Maduka kwenye mji wa Gamagori yaliuza mifuko mitano ya Fugu bila ya kutoa maini yake ambayo ndiyo yenye sumu.

Mifuko mitatu imepatikana lakini mingine miwili bado haijapatikana.

Samaki huyo anadaiwa kuwa na sumu na iwapo makosa kidogo yatafanyika yanaweza kusababisha maafa.

Mamlaka ya mji wa Gamagori katikati mwa Japan imetoa tahadhari na kuwashauri watu kurejesha samaki hao.

Maini ya samaki huyo na ngozi huwa na sumu kali inayoitwa tetrodotoxin na mafunzo maalumu yanahitajika pamoja na lesini kumuandaa samaki huyo.

Hakuna dawa ya kutibu sumu ya samaki huyo.

Waziri Ummy ashtushwa na mrundikano wa wagonjwa Temeke

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameahidi kuongeza idadi ya madaktari bingwa kutoka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ili kuongeza nguvu kwenye Hospitali ya Rufaa ya Temeke .

Waziri Ummy ameyasema hayo leo, Jumatatu alipotembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke baada ya kushuhudia mrundikano wa wagonjwa hospitalini hapo huku kukiwa na upungufu mkubwa wa madaktari bingwa pamoja na vifaa tiba.

"Kubwa nililoligundua hapa ni kuna mrundikano wa watu wanaohitaji huduma, hivyo wale madaktari tunaowatoa Muhimbili hususan madaktari bingwa baadhi tutawahamishia hapa ili kusaidiana na madaktari wa Temeke katika kutoa huduma bora kwa watu wengi zaidi" alisema Waziri Ummy.

Aidha Waziri Ummy amesema kuwa, Serikali ipo mbioni kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya kujenga jengo la ghorofa nne mapema mwaka huu, ambalo litachangia katika kuondoa tatizo la mrundikano wa wagonjwa hospitalini hapo.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke,  Dkt. Amani Malima amesema kuwa wapo mbioni kuagiza vifaa na vifaa tiba kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa wengi wanaojitokeza kwenye hospitali hiyo.

Lowassa afunguka, adai Magufuli alimwita kumshawishi arudi CCM

Waziri Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Edward Lowassa amefunguka na kuzungumzia kile walichozungumza na Rais  John Magufuli huku akisema moja muhimu aliloombwa na kiongozi huyo wa CCM ni kumshawishi arejee Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mgombea huyo wa urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kwenye Uchaguzi wa mwaka 2015 katika taarifa yake iliyotumwa kwa vyombo vya habari amenukuliwa akisema baada ya ombi hilo alimkatalia na kumwambia alijiunga CHADEMA si kwa kubahatisha.

Katika taarifa hiyo, pia Lowassa amesema, licha ya mazungumzo hayo, yeye binafsi pia alipata nafasi ya kumweleza kiongozi huyo wa nchi, kuhusu malalamiko ya wananchi kulalamikia hali mbaya ya uchumi, masuala ya uminywaji wa katiba pamoja na uonevu unaofanywa kwa viongozi wa upinzani ikiwemo kufunguliwa mashtaka pamoja na kupigwa risasi na watu kupotea.

Januari 9, 2017, Lowassa alifika Ikulu na kukutana na Magufuli na kufanya mazungumzo yao ya faragha na baadaye alizungumza na wanahabari kwa kuwaeleza kuwa amefika kuzungumza na huyo pamoja na kumpongeza kwa kazi nzuri anayoifanya ikiwemo ya kufanikisha miradi mikubwa ambayo itasaidia kutengeneza ajira.

Mwendokasi waua watu 11 huko Biharamulo

Watu kumi na mmoja wamekufa na wengine watano wamejeruhiwa katika ajali iliyohusisha magari matatu ikiwemo gari dogo la kubeba abiria na malori mawili iliyokuwa yakitokea wilayani Biharamulo mkoani Kagera.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Olomi amethibitisha kutokea ajali hiyo na tayari Rais  John Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu kufuatia ajali hiyo

Ajali ambayo imeacha simanzi kubwa miongoni mwa ndugu na familia ukiwa ni muendelezo wa ukosefu wa umakini kwa madereva pindi wanapokuwa barabarani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, SACP Olomi amethibitisha idadi ya vifo pamoja na majeruhi waliotokana na ajali hiyo inayodaiwa kusababishwa na mwendo kasi.

Kamanda huyo amesema, gari hilo la abiria lilikuwa na jumla ya abiria 17 na kati ya hao 11 wamekufa na watano wameruhiwa na wanaendela kupatiwa matibabu katika hospitali ya wilaya ya Biharamuro.

SACP Olomi amesema, chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa gari la abiria ambaye anadaiwa hakutumia akili kwa kutaka kulipita gari la mbele yake bila kuwa makini na hivyo kukutana uso kwa uso na lori .  

AZAM TV App yapakuliwa mara milioni

Azam TV App imefanikiwa kupakuliwa mara milioni moja tangu izinduliwe rasmi miezi saba iliyopita.

App hiyo yenye kuleta matukio mbalimbali, ilianza rasmi Julai mwaka jana na kupitia program tumizi mpakuaji anaweza kushuhudia vipindi mbalimbali vikiwemo vya mbashara kupitia king'amuzi cha AZAM TV kwa kumuwezesha kuangalia chaneli nane zenye picha za viwango vya juu, pamoja na habari mbalimbali.

Mbali na kuweza kushuhudia vipindi hivyo kupitia king'amuzi cha Azam TV mbashara, habari zinazopatikana katika app hiyo ni za lugha ya Kiingereza na Kiswahili kuanzia zile za ndani, kimataifa, siasa, na afya hadi maisha.

Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi hicho, Mhariri mkuu wa kitengo cha Online wa Azam TV, Hassan Mhelela amesema kukua kwa App hiyo ni matokeo ya nguvu ya pamoja na kazi kubwa inayofanywa kwa ushirikiano kati ya wafanyakazi na Uongozi wa AZAM TV.

“Hii ni hatua muhimu kwa Azam TV katika matarajio yetu ya kufikia wateja wetu duniani kote. Kupakuliwa mara milioni moja siyo namba ndogo, kufikia hapa inahitaji mipango mahususi, ubunifu na kuwa na matukio na habari za kuvutia,”  amesema Mhelela.

Mhelela pia amegusia  changamoto ya usumbufu wanaoupata wateja wakati wa kuangalia vipindi mbashara kupitia App hiyo ambapo amesema, “Ni kweli tatizo hilo tumeliona  pamoja na kupokea malalamiko kutoka kwa wateja wetu kuwa kuna wakati App yetu inakuwa nzito au inakwama kwama…lakini tunavyozungumza hivi mafundi wetu wanafanyia kazi matatizo yote yenye kulalamikiwa na muda si mrefu kila kitu kitakuwa sawa.”

“Kwa wateja wetu naweza kusema, kuna mengi mazuri yanakuja, cha muhimu endelea kufurahi,” amesema Mhelela. 

Majaliwa awapa habari njema wakazi wa Mara

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali itahakikisha inakamilisha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara iliyoanza kujengwa mwaka 1980.

Waziri mkuu, ametoa kauli hiyo leo, Jumatatu, Januari 15, wakati  wa ukaguzi wa ujenzi wa hospitali hiyo baada ya kuwasili mkoani Mara kwa ajili ya ziara ya siku saba ya kikazi.

Waziri mkuu amesema, Serikali itakamilisha ujenzi wa jengo hilo kwa awamu, ambapo wataanza na eneo la mapokezi pamoja na vyumba vya madaktari.

Amesema Serikali imedhamiria kuboresha huduma za afya nchini, hivyo amewaomba wananchi waendelee kuiamini na kushirikiana nayo.

Waziri mkuu amesema tayari serikali imetoa shilingi bilioni 1.4 ili ujenzi uendelee. Ujenzi huo ulianza mwaka 1980, ulisimama mwaka 1987 na kuanza tena mwaka 2010.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amekagua Uwanja wa Ndege wa Musoma mkoani Mara ambao unatarajiwa kukarabatiwa na kuwekwa lami.

Amesema kukamilika kwa ukarabati huo wa kiwanja hicho kutafungua fursa za utalii ndani ya mkoa huo ambao umezungukwa na vivutio vingi.

Amesema Serikali imedhamilria kukarabati viwanja mbalimbali vya ndege nchini kikiwemo cha Musoma ili kuboresha huduma za usafiri wa anga.

Viwanja vingine vinavyotarajiwa kukarabatiwa ni Iringa, Kilwa Masoko, Lake Manyara, Lindi, Moshi, Njombe, Tanga, Simiyu, Singida na Songea.

Waziri Mkuu amesema viwanja hivyo kwa sasa vinakarabatiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), ambao wanajenga kwa gharama nafuu na kwa viwango vinavyostahili.

Awali, Meneja wa TANROADS, Mkoa wa Mara, Mhandisi Mlima Ngaila alisema ukarabati huo utafanyika kwa awamu tatu ambapo ya kwanza itahusisha upanuzi wa uwanja na ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege.

Alisema barabara ya kuruka na kutua ndege ina urefu wa kilomita 1.6 na upana wa mita 33 ni ya changarawe, hivyo kusababisha baadhi ya ndege kushindwa kutua.

Pia, Waziri Mkuu alikagua ukarabati wa Shule ya Sekondari ya Ufundi ya Musoma na kwamba ameridhishwa na ukarabati wa miundombinu ya shule hiyo.

“Shule hii ilipewa shilingi bilioni 1.28 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu. Nimekagua jengo la utawala, madarasa, mabweni, jiko, maabara na bwalo, nimeridhika na kazi iliyofanyika.”

Shule hiyo ni miongoni mwa shule 10 kongwe ambazo Serikali iliamua kuzikarabati ili ziweze kurudi kama zamani na kuendelea kutumika.

Hata hivyo Waziri Mkuu aliuagiza uongozi wa Manispaa ya Musoma kushirikiana na uongozi wa shule hiyo katika kutatua baadhi ya changamoto zinazoikabili.

Miongoni mwa changamoto hizo ni malipo ya watumishi wasaidizi wakiwemo wapishi, walinzi na madereva, ambapo aliitaka kuchukua jukumu la kuwalipa watumishi hao badala ya kuacha jukumu hilo kwa Mkuu wa Shule.

Rais Magufuli ampa pole RC Kagera kufuatia ajali iliyoua 11

Rais, John Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Mstaafu, Salum Kijuu kufuatia watu 11 kupoteza maisha katika ajali ya gari iliyotokea katika Kijiji cha Nyangozi, Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera.

Ajali hii imetokea jana tarehe 14 Januari, 2018 majira ya saa 11 jioni baada ya basi dogo la abiria aina ya Nissan Caravan lililokuwa likitoka Kakonko mkoani Kigoma kuelekea Kahama mkoani Shinyanga kuligonga ubavuni lori la mizigo kisha kugongana uso kwa uso na lori jingine na kusababisha vifo vya watu 11 na wengine sita (6) kujeruhiwa.

Rais Magufuli amesema amepokea kwa huzuni na masikitiko makubwa taarifa za vifo vya watanzania hao na amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali mstaafu Salum Kijuu kumfikishia pole kwa familia za marehemu wote, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na vifo hivyo.

“Nimehuzunishwa na kusikitishwa sana na vifo hivi, nawapa pole wafiwa wote, ninawaombea marehemu wapumzike mahali pema na majeruhi wapone haraka ili waweze kuungana na familia zao na kuendelea na shughuli zao za kila siku,”  amesema Rais Magufuli.

Aidha, rais Magufuli amewakumbusha watumiaji wa barabara hasa madereva kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama barabarani na ameviagiza vyombo vinavyohusika kuongeza jitihada za kukabiliana na ajali za barabarani ili kuokoa maisha ya watu na mali zinazopotea kutokana na ajali.