Test
Msaada wa haraka wa uokozi wahitajika kwa waliokwama Msumbiji

Mamlaka nchini Msumbiji zimesema kuwa takribani watu 15,000 wanahitaji msaada wa haraka wa kuokolewa baada ya kukwama kwenye maeneo mbalimbali ya nchi hiyo walipokuwa wakijihifadhi kufuatia athari za kimbunga Idai.

Takribani watu 300 wamethibitika kufariki dunia nchini Msumbiji na Zimbabwe lakini idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka.

Kwenye mji wa bandari wa Beira, watoaji misaada wamesema wamebakiwa na maji safi ya kunywa yanayoweza kutosheleza kwa siku mbili au tatu tu.

Kimbuka kikali cha Idai kilichokuwa kikisafiri kwa kasi ya zaidi ya kilomita 177 kwa saa, sawa na mita 106 kwa saa kiliukumba mji wa Beira Alhamisi iliyopita na kuharibu makazi ya watu sambamba na kusukumia maji kwenye makazi hayo na kufanya sehemu kubwa ya mji huo kufunikwa na maji.

Mashirika ya afya yameonya kuwa ukosefu wa chakula na maji safi unaweza kupelekea hatari mpya ya mlipuko wa magonjwa.

Katibu mkuu UN aguswa na vifo na uharibifu wa kimbunga Idai

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameeleza kusikitishwa kwake na kutokea kwa vifo vya watu, uharibifu wa mali na kuhamishwa kwa watu nchini Zimbabwe kutokana na mvua kubwa na mafuriko yaliyosababishwa na kimbunga cha Tropiki cha Idai.

Guterres ametoa salamu za rambirambi kwa familia za wafiwa, serikali na wananchi wa Zimbabwe kwa tukio hilo la kusikitisha.

Amesema Umoja wa Mataifa uko pamoja na Mamlaka za Zimbabwe na kuwa tayari kutoa msaada wa kibinadamu kufuatia maafa hayo.

Kimbunga Idai kimesababisha vifo vya watu 150 nchini Malawi, Msumbiji na Zimbabwe na mamia ya wengine hawajulikani walipo.

Tanzania katika kuonesha mashikamano na uhusiano mzuri ulionao nan chi hizo imetoa msaada wa vyakula na dawa.

Viongozi Afrika wakubaliana kukabili ongezeko la vijana

Viongozi wa Afrika wamekubaliana kuwepo kwa ongezeko la idadi ya Vijana barani humo jambo ambalo limekuwa likisababisha kuwepo kwa changamoto kadhaa wa kadhaa kwenye mataifa husika.

Kutokana na ongezeko hilo viongozi hao wameona ni vyema kukawa na mkakati wa kuwahusisha kutoa elimu ya kuwawezesha kujiajiri lakini kazi kubwa ikiangaliwa kwenye ukuzaji wa uchumi wa mataifa hayo.

Hayo yameafikiwa leo, katika mkutano wa siku mbili wa Africa Now uliofanyika nchini Uganda Tanzania imewakilishwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kwa niaba ya Rais John Magufuli.

Makamu wa Rais,  Samia Suluhu Hassan amesema kutokana na changamoto hiyo wakati huu ndiyo unawapasa viongozi wa Afrika kuiangalia Afrika ijayo na viongozi wa sasa hawana budi kuandaa mazingira ya Afrika bora na salama.

Makamu wa Rais amesema mkutano huo umeangalia suala zima la ongezeko la watu na uelewa wa vijana katika maendeleo ya nchi zao hususan wakati huu ambapo nchi nyingi zinajipambanua katika uchumi wa viwanda na kuhimiza suala la kuangalia mitaala ya elimu inayotolewa sasa kama inakidhi mahitaji ya kisayansi na kiteknolojia.

“Lazima sasa tuangalie hii idadi ya watu isije ikawa chanzo cha kuleta vurugu katika nchi zetu bali iwe chanjo cha nguvu kazi kujenga nchi zetu,”alisema Makamu wa Rais.

Makamu wa Rais amesisitiza kuwa Afrika ya sasa inahitaji Viongozi ambao hawajitazami wao bali wanatazama wananchi wao katika makundi yao kama Vijana, Wanawake na Walemavu.

Makamu wa Rais pia alikutana na kuzungumza na Naibu Rais wa Kenya, William Ruto ambapo baada ya kikao hicho Makamu wa Rais amesema Tanzania na Kenya ni majirani pamoja na kuwa kwenye jumuiya ya Afrika Mashariki lakini wao kama nchi jirani lazima wahakikishe uhusiano wao unasimama imara na kukuza ushirikiano.

Bouteflika akubali yaishe, ajiondoa kuwania urais Algeria

Rais wa Algeria, Abdelaziz Bouteflika aliyetangaza awali kuwania kipindi cha tano cha urais wa nchi hiyo ametangaza kuahirisha nia yake hiyo na kwamba hatagombea tena nafasi hiyo.

Abdelaziz Bouteflika ambaye ameiongoza Algeria kwa miaka 20 ameahirisha uchaguzi huo uliokuwa ufanyike Aprili 18 na kuitaka tume ya uchaguzi kupanga tarehe mpya ya uchaguzi wa nchi hiyo.

Hatua hiyo imepokelewa kwa shangwe na wananchi wa Algeria ambao walifanya maandamano ya majuma kadhaa kupinga kiongozi wao huyo ambaye hajaonekana hadhara kwa kipindi kirefu tangu apate maradhi ya kiharusi mwaka 2013, kuwania tena nafasi hiyo wakidai wanataka kiongozi atakayekuwa na fikra mpya na mwenye afya na uwezo wa kuongoza.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Bouteflika, tayari tarehe ya uchaguzi mpya imeshapangwa na mabadiliko ya baraza la mawaziri yatatangazwa muda si mrefu.

Katika hatua nyingine, Waziri mkuu wa nchi hiyo, Ahmed Ouyahia ametangaza kujiuzuru na nafasi yake kuchukuliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Noureddine Bedoui, ambaye amepewa jukumu la kuunda serikali mpya, Kwa mujibu wa Shirika la Habari la APS.

Haijawekwa wazi kama kiongozi huyo aliyewahi kuwa kipenzi cha WaAlgeria atajiuzuru kabla ya muda wake ama la kupisha serikali hiyo mpya kabla ya uchaguzi.

Samia Suluhu amwakilisha JPM kwenye mkutano wa 'AFRICA NOW'

Makamu wa Rais, Samia Hassan Suluhu anaondoka leo nchini kwa ajili ya kwenda kuhudhuria mkutano wa AFRICA NOW SUMMIT unaotarajiwa kufanyika jijini Kampala nchini Uganda. Katika mkutano huo Makamu wa Rais anakwenda kumwakilisha Rais, John Magufuli.

Katika mkutano huo wa siku mbili unaotarajiwa kuanza kesho Jumanne, Machi 12 na 13, mada ya viongozi wa Afrika kuleta chachu ya maendeleo endelevu barani Afrika ndiyo itakayozungumziwa huku makamu wa Rais akiwasilisha mada ya uongozi unaotakiwa kuchochea mabadiliko ya kijamii na uchumi Afrika.

Wengine wanaotarajiwa kutoa mada katika mkutano huo mbali na makamu wa Rais, ni pamoja na  Rais wa Misri ambaye pia ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Abdel Fattah el Sisi, Rais wa Afrika kusini, Cyril Ramaphosa, Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto na Waziri mkuu wa Ethiopia, Ahmed Abiy.

Katika mkutano huo, viongozi hao watajikita katika kujadili uongozi wenye kuleta chachu ya maendeleo na utafunguliwa na mwenyekiti wa mkutano huo, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni  huku Rais wa Somalia, Mohamed Abdullahi akitarajiwa kufunga mkutano huo kwa hotuba kama ya kufungwa rasmi na Rais Yoweri Kaguta.

Maelfu ya abiria wakwama kusafiri JKIA Kenya

Maelfu  ya abiria wamejikuta wakiwa hawajui la kufanya katika viwanja vyote vinne nchini Kenya baada ya kutokea mgomo wa wafanyakazi uliosababisha usumbufu mkubwa wa ndege.

Wafanyakazi hao waliogoma leo wamesema, hawajafurahia kuhusu mpango wa kuziunganisha mamlaka za viwanja vya ndege na Shirika la Ndege la Taifa.

Takribani ndege 60 zimeshindwa kupaa leo, Jumatano kutoka kwenye Uwanja huo wa ndege wa Kimataifa wa  Jomo Kenyatta ambao ni uwanja mkubwa zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki na kulazimika kutua katika Uwanja wa ndege wa Mwl. Julius Nyerere Dar es Salaam.  Huku kukidaiwa kuwepo kwa baadhi ya ndege kukosa abiria kabisa.

Viwanja vya ndege vya Mombasa, Eldoret na Kisumu nazo pia zimedaiwa kupatwa na usumbufu huo.

Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta imelaani mgomo huo na kusema ni kinyuma na sheria.  Aidha imesema, utaratibu unafanyika wa kuwapeleka watumishi wengine kuweka sawa hali iliyopo.

Inasemekana kuwa, polisi wamepelekwa katika uwanja wa ndege wa Nairobi na kuwarushia mabomu ya machozi wafanyakazi hao waliokuwa katika mgomo.

Kiongozi mkuu aliyeratibu  mgomo huo kutoka Chama cha Umoja wa wafanyakazi wa Mamlaka ya Anga nchini Kenya ambaye ni Katibu mkuu, Moss Ndiema, amekamatwa.

Buhari aongoza matokeo ya awali kura za urais Nigeria

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria anaonekana kuongoza katika matokeo ya awali ya kura zinazoendelea kuhesabiwa za uchaguzi wa Rais ambao hadi sasa unakumbwa na shutma nzito za wizi wa kura.

Buhari anaonekana kuongoza katika majimbo saba kati ya 36 wakati mshindani wake Atiku Abubakar amenyakua majimbo manne katika mji mkuu wa Abuja.

Kiongozi wa PDP, Uche Secondes amekishutumu Chama cha Rais Buhari cha APC kimekuwa kikitumia maofisa wa juu wa tume ya uchaguzi nchini humo INEC kubadili matokeo ambayo amedai chama chake kinaongoza.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari Secondes amesema anaamini chama chake kinaongoza ila Rais Buhari amekuwa akiweka shinikizo kubwa ndani ya tume na huko ni kukiukwa kwa sheria ya uchaguzi katika zoezi hilo.

"Chama cha PAC kwa kushirikiana na APC wamechukua hatua ambazo si za kiungwana, hasa katika kuhonga, kulaghai, kuweka vizuizi, wakitumia vyombo vya ulinzi na usalama hasa polisi, na jeshi."

Seconds amesema kumekuwepo na jaribio la serikali kubadili matokeo ya uchaguzi huo japo hakuwa na ushahidi wa moja kwa moja.

Rais Buhari anayetetea kiti chake amewasihi wananchi wa taifa hilo kuwa watulivu katika kipindi hiki kura zikihesabiwa  na ulinzi kuimarishwa lakini hakuacha pia kumtupia lawama upinzani wake hasa Chama cha PDP kujaribu kutaka kuchezea matokeo hayo.

Matokeo ya mwisho yanataraji kutangazwa mwishoni mwa juma hili japo haijawekwa wazi ni lini hasa.

Katika hatua nyingine watu wawili wanashikiliwa na polisi nchini humo wakihusishwa na vifo vya watu takribani 47 ambao asasi za kiraia wanadai vilitokana na vurugu za uchaguzi.

Rais Buhari anatetea kiti chake katika n’gwe nyingine ambapo endapo atashinda amewaahidi Wananchi hao kuendeleza yale aliyoyafanya katika kipindi chake cha uongozi.