Test
Prince Harry na Meghan kuzawadia watoto wengine zawadi za mtoto wao

Mwanamfalme Harry na mkewe Meghan Markle wameonesha furaha na mapenzi yao kwa pamoja katika ukurasa wao wa Instagram kwa kuwataka mashabiki wao kutoendelea kutuma zawadi  kwaajili ya mtoto wao mtarajiwa na badala yake zawadi hizo zitumwe kwenye vituo vya uhutaji vilivyochaguliwa.

Watawala hao wa eneo wa Sussex wametoa pendekezo hilo  kupitia  ukurasa wao huo wa pamoja wa Instagram kufuatia kufurika kwa zawadi na salamu za mtoto mtarajiwa anayetarajiwa kuzaliwa wiki chache zijazo mwezi huu.

Katika pendekezo lao hilo wawili hao wameshukuru kwa michango ya salamu na zawadi zinazomiminika kwao ambazo mpaka sasa jumla ya wanasesere 90 na vinguo aina ya vifulana 15 vimeshapokelewa katika kasri lao.

Kupitia ukurasa huo uliozinduliwa Alhamisi ya juma hili, na tayari umeshafikia wafuasi milioni 4.1 wawili hao wamewataka wapenzi na wafuasi wao kuchangia kwenye vituo vinne walivyopendekezwa zawadi hizo kupelekewa na baadaye kuzisambaza kwa watoto na wazazi wenye uhitaji mbalimbali.

Wawili hao wamewashukuru wafuasi na wapenzi wao kwa salamu na mapenzi waliyoyaonesha kwao wakati huu ambao wanasubiri mtoto wao wa kwanza.

Taarifa hiyo ilisisitizwa pia kupitia taarifa kwa umma ikisisitiza Umma kuchangia vituo vyenye uhitaji na kuchangia huko na kuwashukuru wote ambao wameshachangia .

Vituo ambavyo vimeteuliwa ni pamoja na taasisi zifuatazo ambazo ni The LunchboxFund, Littlevillagehg, WellChild na Baby2Baby.

Mwanamke ajifungua juu ya mti akikwepa mafuriko ya kimbunga Idai, Msumbiji

Mwanamke mmoja wa Msumbiji ameingia kwenye kumbukumbu muhimu za dunia baada ya kufanikiwa kujifungua salama akiwa juu ya mti wakati akiyakwepa mafuriko.

Mwanamke huyo Amelia amefanikiwa kujifungua mtoto wa kike aliyempa jina la Sara, wakati akining’inia kwenye matawi ya mti wa mwembe akiwa na mtoto wake mdogo wa kiume.

Familia hiyo ya watu watatu iliokolewa siku mbili zilizofuata na majirani zake.

Amelia na majirani zake walitafuta hifhadhi kwenye sehembu mbalimbali kufuatia kimbunga cha Idai kilichoua watu zaiid ya 700.

Kitendo cha mwanamke kujifungua juu ya mti kimekuja miaka 20 baada ya tukio kama hilo kutokea nchini humo ambapo msichana Rosita Mabuiango alipozaliwa juu ya mti wakati mafuriko yalipoikumba sehemu ya kusini mwa Msumbiji.

"Nilikuwa nyumbani na mtoto wangu wa kiume mwenye miaka miwili, ghafla na bila ishara yoyote, maji yakaanza kuingia ndani ya nyumba yetu," Amelia ameliambia Shirika la Umoja wa Mataifa la watoto (UNICEF).

Rais Magufuli afanya uteuzi Wizara ya Fedha, TRA

Rais Magufuli amemteua Adolf Hyasinth Mohondela Ndunguru kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango anayeshughulikia Sera.

Ndunguru ameteuliwa kushika nafasi ya Naibu  Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango (Sera) ambayo ilikuwa wazi.

Kabla ya uteuzi huo, Ndunguru alikuwa Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Kufuatia Uteuzi huo, Rais Magufuli amemteua Msafiri Lameck Mbibo kuwa Naibu Kamishna Mkuu wa TRA.

Kabla ya Uteuzi huo, Mbibo alikuwa Meneja wa TRA Mkoa wa Kilimanjaro.

Uteuzi wa viongozi hao unaanza mara moja leo tarehe 31 Machi, 2019.

 

Aliyetangazwa “kufariki” tangu Disemba ajifungua mtoto

Mwanamichezo wa kimataifa, Catarina Sequeira (26) aliyetangazwa na jopo la madaktari nchini Ureno kuwa ni mfu wa ubongo tangu Disemba mwaka jana, amejifungua mtoto wa kiume siku ya Alhamisi.

Mtoto huyo aliyepewa jina la Salvador, amezaliwa akiwa na uzito wa kilo 1.7kg baada ya kukua kwa wiki 32 tumboni mwa mama yake, na sasa yupo chini ya uangalizi katika moja ha hospitali ya watoto nchini humo.

Sequeira amezikwa Ijumaa, siku moja baada ya mtoto kutolewa tumboni mwake.

Mama mzazi wa Sequeira, Maria de Fátima Branco, ameiambia televisheni moja ya Ureno kuwa alimuaga binti yake Disemba 26, na uamuzi wa kumuacha mtoto huyo azaliwe ulifikiwa kutokana na shauku ya muda mrefu ya baba wa mtoto (Salvador), Bruno, kuhitaji mtoto.

Hii ni mara ya pili nchini Ureno kwa mtoto kuzaliwa kutoka kwa mama ambaye ni 'mfu wa ubongo'.

Sequeira ambaye alikuwa mwanariadha wa mbio za mitumbwi amekuwa akisumbuliwa na pumu toka utoto wake.

Shambulio lililochukua uhai wake lilimpata akiwa na mimba ya wiki 19, hali iliyomfanya kupoteza fahamu.

Siku chache akiwa chumba cha wagonjwa mahututi hali ilizidi kuwa mbaya na akatangazwa kuwa 'mfu wa ubongo' Disemba 26. Madaktari wakamuwekea mashine ya kusaidia kupumua ili mtoto tumboni aweze kuishi. Mashine hiyo iliwekwa kwa siku 56.

Chanzo: BBC

 

Dkt. Sambaiga ateuliwa kuwa mwenyekiti wa Bodi mashirika yasiyo ya kiserikali

Rais John Magufuli amemteua Dkt. Richard Faustine Sambaiga kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi wa Dkt. Sambaiga umeanza rasmi Machi, 23.

Dkt. Sambaiga ni Mhadhiri Mwandamizi, Idara ya Sosholojia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Rukia Masasi ambaye amemaliza muda wake.

Wakati huo huo, Rais Magufuli kesho Machi, 28 atamuapisha Balozi Mteule Valentino Mlowola kuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba.

Balozi Mteule Mlowola ataapishwa Ikulu Jijini Dar es Salaam, kuanzia saa 3:30 asubuhi.

Tanzania miongoni mwa nchi zenye tatizo la lishe duni

Tanzania ni moja kati ya nchi ambazo zinakabiliwa na  tatizo la lishe duni hususani kwa watoto wenye umri chini ya miezi sita hadi 59 pamoja na akina mama ambao wananyonyesha jambo linalosababisha watoto wengi kudumaa.

Akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam Binti Mfalme wa  Jordan,  Saraah Zeid amesema moja kati ya sababu zinazosababisha lishe duni ni umaskini.

Kufuatia hilo binti mfalme huyo amesena ameamua kufika nchini kuendeleza program mbalimbali za kuwawezesha wananchi kuzingatia lishe hiyo ikiwa ni pamoja na kuanzisha vikundi vya kina mama vya kukopeshana ambapo hadi sasa wanatekeleza program hizo katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Singida na Dodoma.

Zitto ayataka matawi ya ACT Wazalendo kuorodhesha wanachama wao

Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amewataka viongozi wa matawi kuorodhesha majina ya wanachama wao katika matawi waliyopo na kuwatambua huko huko ili kuepusha vurugu zisizo za lazima. 

Kauli hiyo ameitoa katika ofisi za makao makuu ya chama hicho iliyopo Kijitonyama Dar es Salaam mara baada ya kuzuiwa na Jeshi la Polisi kufanya mkutano huo ambao walipanga kuufanya katika Ukumbi wa PR Stadium Temeke kupokea wanachama wapya 12,600.

Mkutano huo wa kupokea wanachama ulihudhuriwa pia na viongozi mbalimbali akiwemo aliyekuwa makamu wa Rais wa kwanza  wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad na viongozi wengine ambapo wamepokea kadi zaidi ya 900.