Test
Makamu wa Rais awataka Wazanzibar kuilinda miundombinu iliyopo

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi kuendelea kuenzi miundombinu iliyosimamiwa na kutekelezwa chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein.

Makamu wa Rais huyo amesema hayo wakati wa ufunguzi wa kongamano la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) la kumpongeza Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Shein lililoratibiwa na umoja huo kwa upande wa Tanzania Bara na Visiwa.

Makamu wa Rais amewataka wananchi wa visiwani humo kuhakikisha wanasimamia na kuilinda miundombinu na maendeleo yaliyofikiwa chini ya uongozi wa Dkt. Shein ili iweze kudumu kwa maslahi ya wananchi wote na vizazi vijavyo.

Wakati huo huo, makamu wa Rais, amewataka wanawake kuhakikisha wanafanyakazi kwa bidii na kuzisemea kazi nzuri zinazofanywa na viongozi wa pande zote mbili ili wananchi wazijue na wasipotoshwe.

“Sisi ni sehemu muhimu sana ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi, hivyo Kongamano hili liwe chachu yetu katika kuchapa kazi zaidi.

"Sote ni mashuhuda wa kazi kubwa na nzuri iliyofanyika hapa Zanzibar kwa kipindi cha miaka mitatu. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Uongozi mahiri wa Dokta Shein imefanya kila liwezekanalo kuboresha hali ya maisha ya wananchi wa Zanzibar kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta zote za kijamii, kisiasa na kiuchumi.”Alisisitiza Makamu wa Rais.

Profesa Lipumba amtangaza mrithi wa Maalim Seif Shariff Hamad

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amemtangaza Khalifa Suleiman Khalifa kuwa katibu mkuu wa chama hicho akichukua nafasi ya Maalim Seif Sharrif Hamad.

Mbali na Khalifa, Profesa Lipumba pia amemtangaza Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya kuwa Naibu Katibu mkuu Bara na Fakhi Suleiman Khatibu kuwa Naibu Katibu mkuu Zanzibar.

Profesa Lipumba amemtangaza Khalifa ambaye ni mbunge wa zamani wa Gando kuchukua nafasi ya Maalim Seif Sharif Hamad leo, Jumamosi baada ya kiongozi hao kushindwa kufikia muafaka wa kufanya kazi pamoja na hivyo kila upande kujigawa kwa kuwa na wafuasi wake.

Viongozi hao wamepatikana baada ya kuchaguliwa na Baraza Kuu la Uongozi lililokutana jana Ijumaa.

Hata hivyo, hatima ya viongozi hao wapya wa CUF akiwamo Profesa Lipumba aliyechaguliwa na mkutano mkuu Jumatano iliyopita Machi 14, 2019, itajulikana baada ya hukumu itakayotolewa Jumatatu ya Machi 18, 2019 na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam.

Hukumu hiyo ni ya kesi iliyofunguliwa na baadhi ya wanachana wa chama hicho upande wa Maalim Seif wakipinga uhalali wa Profesa Lipumba kuwa Mwenyekiti wa CUF.

Jimbo la Joshua Nasari latangazwa kuwa wazi

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungana wa Tanzania, Job Ndugai amemuandika barua, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Semistocles Kaijage kuwa Jimbo la Arumeru Mashariki kwa sasa liko wazi kufuatia, Mbunge wake Joshua Nasari ( CHADEMA) kushindwa kuhudhuria mikutano mitatu mfululizo na hivyo kupoteza sifa za kuendelea kuwa mbunge.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Spika Ndugai amesema, Mbunge Nasari hajahudhuria vikao hivyo vitatu mfululizo kikiwemo cha Mkutano wa kumi na kumi na mbili wa tarehe 4 -14 Septemba 2018 na mkutano wa kumi na tatu wa tarehe 6- 16 Novemba mwaka 2018.

Mkutano mwingine ambao Nasari anadaiwa hajahudhuria ni wa kumi nne wa tarehe 29 Januari  hadi Februari 9, 2019.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uamuzi huo wa spika umezingatia masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 71 (1) C ambayo inaeleza kuwa, “mbunge atakoma kuwa mbunge na ataacha kiti chake katika Bunge ikiwa atakosa kuhudhuria vikao vya mikutano vya Bunge mfulululizo bila ya ruhusa ya spika.”

Kanuni hiyo pia ikisaidiwa na ile ya 146 (1) na (2)  za Kanuni za Kudumu za Bunge toleo la Januari 2016. Kutokana na taarifa hiyo Tume ya Uchaguzi inaweza kuendelea na mchakato wa kupata Mbunge wa kujaza nafasi hiyo iliyo wazi katika Jimbo hilo la Arumeru Mashariki.  

Viongozi Afrika wakubaliana kukabili ongezeko la vijana

Viongozi wa Afrika wamekubaliana kuwepo kwa ongezeko la idadi ya Vijana barani humo jambo ambalo limekuwa likisababisha kuwepo kwa changamoto kadhaa wa kadhaa kwenye mataifa husika.

Kutokana na ongezeko hilo viongozi hao wameona ni vyema kukawa na mkakati wa kuwahusisha kutoa elimu ya kuwawezesha kujiajiri lakini kazi kubwa ikiangaliwa kwenye ukuzaji wa uchumi wa mataifa hayo.

Hayo yameafikiwa leo, katika mkutano wa siku mbili wa Africa Now uliofanyika nchini Uganda Tanzania imewakilishwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kwa niaba ya Rais John Magufuli.

Makamu wa Rais,  Samia Suluhu Hassan amesema kutokana na changamoto hiyo wakati huu ndiyo unawapasa viongozi wa Afrika kuiangalia Afrika ijayo na viongozi wa sasa hawana budi kuandaa mazingira ya Afrika bora na salama.

Makamu wa Rais amesema mkutano huo umeangalia suala zima la ongezeko la watu na uelewa wa vijana katika maendeleo ya nchi zao hususan wakati huu ambapo nchi nyingi zinajipambanua katika uchumi wa viwanda na kuhimiza suala la kuangalia mitaala ya elimu inayotolewa sasa kama inakidhi mahitaji ya kisayansi na kiteknolojia.

“Lazima sasa tuangalie hii idadi ya watu isije ikawa chanzo cha kuleta vurugu katika nchi zetu bali iwe chanjo cha nguvu kazi kujenga nchi zetu,”alisema Makamu wa Rais.

Makamu wa Rais amesisitiza kuwa Afrika ya sasa inahitaji Viongozi ambao hawajitazami wao bali wanatazama wananchi wao katika makundi yao kama Vijana, Wanawake na Walemavu.

Makamu wa Rais pia alikutana na kuzungumza na Naibu Rais wa Kenya, William Ruto ambapo baada ya kikao hicho Makamu wa Rais amesema Tanzania na Kenya ni majirani pamoja na kuwa kwenye jumuiya ya Afrika Mashariki lakini wao kama nchi jirani lazima wahakikishe uhusiano wao unasimama imara na kukuza ushirikiano.

Bouteflika akubali yaishe, ajiondoa kuwania urais Algeria

Rais wa Algeria, Abdelaziz Bouteflika aliyetangaza awali kuwania kipindi cha tano cha urais wa nchi hiyo ametangaza kuahirisha nia yake hiyo na kwamba hatagombea tena nafasi hiyo.

Abdelaziz Bouteflika ambaye ameiongoza Algeria kwa miaka 20 ameahirisha uchaguzi huo uliokuwa ufanyike Aprili 18 na kuitaka tume ya uchaguzi kupanga tarehe mpya ya uchaguzi wa nchi hiyo.

Hatua hiyo imepokelewa kwa shangwe na wananchi wa Algeria ambao walifanya maandamano ya majuma kadhaa kupinga kiongozi wao huyo ambaye hajaonekana hadhara kwa kipindi kirefu tangu apate maradhi ya kiharusi mwaka 2013, kuwania tena nafasi hiyo wakidai wanataka kiongozi atakayekuwa na fikra mpya na mwenye afya na uwezo wa kuongoza.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Bouteflika, tayari tarehe ya uchaguzi mpya imeshapangwa na mabadiliko ya baraza la mawaziri yatatangazwa muda si mrefu.

Katika hatua nyingine, Waziri mkuu wa nchi hiyo, Ahmed Ouyahia ametangaza kujiuzuru na nafasi yake kuchukuliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Noureddine Bedoui, ambaye amepewa jukumu la kuunda serikali mpya, Kwa mujibu wa Shirika la Habari la APS.

Haijawekwa wazi kama kiongozi huyo aliyewahi kuwa kipenzi cha WaAlgeria atajiuzuru kabla ya muda wake ama la kupisha serikali hiyo mpya kabla ya uchaguzi.

UVCCM watetea uamuzi wa Lowassa, wadai ni somo kwa vijana

Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umesema kuwa uamuzi wa kumpokea Waziri Mkuu Mstaafu na aliyekuwa Mgombea Urais kupitia Chadema, Edward Lowassa, umefuata taratibu sawa na wanachama wengine lakini pia umetoa somo kwa vijana kufahamu hakuna mkamilifu kwenye safari ya kisiasa.

Hayo yamesemwa jijini Dodoma na  Mwenyekiti wa UVCCM, Kheri James, ambapo amesema kama Lowassa angepokelewa kinyume na chama hicho, umoja huo ungesimama kukemea.

“Tunawapongeza viongozi wakuu wa Chama kwa kitendo cha kumpokea Lowassa. amerudi CCM kwa kuzingatia taratibu zote kama wanachama wengine. Lowassa ni raia wa Tanzania kuhamia Chadema hakumuondolei haki ya kurejea CCM,” amesema James

Amesema kuwa milango ipo wazi kwa wanasiasa wengine wenye kutaka kuhamia CCM kwani mtaji wa chama chochote cha siasa ni wanachama.

Aidha, Mwenyekiti huyo ambaye aliambatana na viongozi waandamizi wa UVCCM, amesema viongozi wa kisiasa wanapaswa kuwa watiifu kwa sheria za nchi.

Hata hivyo ametangaza mchakato wa kuziba nafasi ya aliyekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) upande wa vijana, Sophia Kizigo ambaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma.

Samia Suluhu amwakilisha JPM kwenye mkutano wa 'AFRICA NOW'

Makamu wa Rais, Samia Hassan Suluhu anaondoka leo nchini kwa ajili ya kwenda kuhudhuria mkutano wa AFRICA NOW SUMMIT unaotarajiwa kufanyika jijini Kampala nchini Uganda. Katika mkutano huo Makamu wa Rais anakwenda kumwakilisha Rais, John Magufuli.

Katika mkutano huo wa siku mbili unaotarajiwa kuanza kesho Jumanne, Machi 12 na 13, mada ya viongozi wa Afrika kuleta chachu ya maendeleo endelevu barani Afrika ndiyo itakayozungumziwa huku makamu wa Rais akiwasilisha mada ya uongozi unaotakiwa kuchochea mabadiliko ya kijamii na uchumi Afrika.

Wengine wanaotarajiwa kutoa mada katika mkutano huo mbali na makamu wa Rais, ni pamoja na  Rais wa Misri ambaye pia ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Abdel Fattah el Sisi, Rais wa Afrika kusini, Cyril Ramaphosa, Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto na Waziri mkuu wa Ethiopia, Ahmed Abiy.

Katika mkutano huo, viongozi hao watajikita katika kujadili uongozi wenye kuleta chachu ya maendeleo na utafunguliwa na mwenyekiti wa mkutano huo, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni  huku Rais wa Somalia, Mohamed Abdullahi akitarajiwa kufunga mkutano huo kwa hotuba kama ya kufungwa rasmi na Rais Yoweri Kaguta.