Ligi ya Mabingwa Afrika: Simba yairarua Mbabane Swallows

|
Meddie Kagere, mfungaji wa bao la tatu la Simba kwenye mchezo uliomalizika kwa Simba kushinda 4-1 dhidi ya Mbabane Swallows kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Mabingwa wa Tanzania Bara Simba SC wameianza kwa kicheko Ligi ya Mabingwa barani Afrika Caf Champions League (CafCL) kwa kuipa Mbabane Swallows kichapo cha mabao 4-1 katika mchezo wa kwanza wa hatua ya awali ya ligi hiyo uliopigwa leo kwenye Dimba la Taifa Dar es Salaam.

Nahodha wa Simba John Bocco amefunga mabao mawili, akianza la kwanza dakika ya 8 ya mchezo, na bao la pili akilifunga kwa mkwaju wa penati baada ya Emmanuel Okwi kuangushwa ndani ya eneo la hatari.

Simba ilipata mabao yake mengine kipindi cha pili kupitia kwa Meddie Kagere aliyefunga bao la tatu dakika ya 84 akitumia vyema makosa yaliyofanywa na kipa wa Mbabane Swallows ambaye aliteleza na kushindwa kudhibiti mpira aliorejeshewa na beki wake kabla ya Kagere kuuwahi na kuusukumiza nyavuni.

Bao la nne lilifungwa na Clatous Chama dakika za majeruhi akitumia vyema pasi ya Hassan Dilunga aliyeingia dakika ya 86 kuchukua nafasi ya John Bocco.

Bao pekee la Mbabane limefungwa na Guevane Nzambe dakika ya 24 kwa shuti kali akitumia makossa ya mabeki wa Simba waliopoteza umakini katika eneo lao kufuatia mpira wa kona wa Mbabane Swallows.

Matokeo haya yanaiweka Simba mahali pazuri kufuzu hatua inayofuata, kwani itahitaji sare aina yoyote kufuzu au kipigo cha mabao yasiyozidi 3-0. Mechi ya marudiano ni Desemba 5 nchini eSwatin.

CAF
Maoni