Test
Rais Magufuli akutana na uongozi mpya wa Barrick

Rais John Magufuli leo, Jumatano Februari, 20 amekutana na kufanya mazungumzo na Afisa Mwendeshaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick Gold anayeshughulikia Afrika na Mashariki ya Kati, Dkt. Willem Jacobs, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Baada ya mazungumzo hayo Dkt. Willem Jacobs aliyeongozana na washauri wa Barrick Gold Corporation ambao ni Rich Haddock, Duncan Bullivant na Wicus du Preez amesema wamekutana na Rais Magufuli ili kumhakikishia kuwa makubaliano yaliyofikiwa Oktoba, 19, 2017 watayatekeleza kikamilifu hasa baada ya kampuni kubwa ya uchimbaji dhahabu ya Rand Gold ya Afrika Kusini kuungana na Barrick Gold Corporation katika umiliki, uwekezaji na menejimenti.

Dkt. Willem Jacobs amebainisha kuwa hakuna kitakachokuwa tofauti na makubaliano yaliyofikiwa awali ambayo yaliongozwa na Mwenyekiti Mtendaji wa Barrick Gold Corporation, Prof. John Thornton ikiwemo Barrick Gold Corporation kuilipa Serikali ya Tanzania kifuta machozi cha Dola za Marekani Milioni 300 (sawa na shilingi Bilioni 682.5), kuendelea na uwekezaji kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Barrick Gold na mgawanyo wa mapato ya kiuchumi kwa uwiano wa asilimia 50 kwa 50 kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Barrick Gold.

Dkt. Willem Jacobs amempongeza Rais Magufuli kwa jitihada zake za kusimamia maslahi ya Watanzania katika rasilimali za nchi yao na amesema pamoja na ukweli kwamba Rais Magufuli yupo katika njia sahihi, yeye akiwa Mwafrika anaunga mkono juhudi hizo kwa kuwa ndiyo mwelekeo sahihi ambao nchi za Afrika zinapaswa kuufuata.

“Mimi ni Mwafrika na sisi sote ni Waafrika, anachokifanya Mhe. Rais Magufuli ni sahihi kabisa, anahakikisha utajiri wa rasilimali uliopo unabainishwa na unawanufaisha Watanzania na ndiyo maana tupo hapa kwa sababu tunakubaliana na Mhe. Rais.

Na hivi ndivyo sisi Waafrika tunapaswa kufanya kwa rasilimali zetu, na sisi tunahakikisha tunafanya kazi vizuri na Serikali na jamii kulinda rasilimali hizi, kumbuka rasilimali hizi ni za wananchi, jukumu langu kama mwekezaji ni kubadili hayo madini kuwa kodi na ajira kwa Tanzania na pia kampuni yangu kupata faida yake halali” amesema Dkt. Willem Jacobs.

Amebainisha kuwa baada ya muungano huo wa Rand Gold na Barrick Gold, sasa Kampuni mpya ya Barrick Gold imekuwa kampuni kubwa inayoongoza kwa umiliki wa rasilimali za dhahabu duniani ikimiliki rasilimali 5 kati ya 10, na kwamba kutokana na uwezo huo Barrick Gold Corporation sasa imeweza kujiimarisha zaidi kiuwekezaji na utaalamu na ipo tayari kushirikiana na Tanzania kuhakikisha rasilimali ya dhahabu iliyopo inaleta manufaa kwa pande zote mbili yaani Watanzania na mwekezaji.

Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi ambaye ameongoza timu ya majadiliano kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Barrick Gold amesema nyaraka za makubaliano hayo zimekamilika na kwamba sasa kinachosubiriwa ni utekelezaji wa makubaliano hayo unaotarajiwa kukamilika ifikapo mwisho wa mwezi Machi 2019.

“Baada ya muungano wao (Rand Gold na Barrick Gold Corporation) hii sasa ni timu mpya na tumewaona ni watu ambao sasa wapo tayari kutekeleza yale yote yaliyokubaliwa, na sasa ni kwa kila upande kwenda kwenye vyombo vyake vinavyohusika kufanya maamuzi ya mwisho ili utekelezaji ufanyike” amesema Prof. Kabudi.

Makisio ya bajeti ya fedha 2019/20 yapungua Nyang'hwale

Katika Makisio na matumizi ya bajeti ya mwaka wa fedha 2019/2020 kwa mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita yameonekana kupungua  kutoka bilioni 1.4 hadi milioni 832.19 ambayo ni sawa na  asilimia 40.6

Kushuka kwa makadirio hayo ni kutokana na kupungua kwa mapato katika chanzo kikubwa kilichokuwa kikitegemewa na Halmashauri hiyo ambacho ni kodi ya huduma kutoka mgodi wa Bulyanhulu uliopo chini ya Kampuni ya Accaci ambayo uzalishaji wake unadaiwa kupungua kwa asilimia 90.

Akiwasilisha mapendekezo ya rasimu ya mpango  na bajeti ya halmashauri kwa mwaka ujao wa fedha 2019/2020 katika mkutano maalum wa Baraza la Madiwani Afisa Mipango amesema mbali na chanzo hicho pia zao la pamba makisio yake yamepungua kutoka milioni 406 kwa mwaka huu wa fedha 2018/2019 hadi kufikia  milioni 125.

Kutokana na kushuka kwa nyanzo vya ndani vya mapato halmashauri hiyo imebuni vyanzo vipya ambavyo vitaanza kukusanya mwaka ujao wa fedha vikiwemo ushuru wa minara, ushuru wa madini ya ujenzi na chanjo ya mifugo

Makatibu wanane wa wizara watembelea chanzo cha mto Ruaha

Jumla ya makatibu wakuu wanane (8) kutoka wizara tofauti wanaounda timu maalumu inayofuatilia uandaaji wa mapendekezo yatakayosaidia kutafuta suluhu ya changamoto za migogoro ikiwa ni pamoja na mwendelezo wa utekelezaji wa agizo la rais kuhakikisha vijiji vilivyosajiliwa na  vilivyomo ndani ya hifadhi vinarasimishwa.

Katika eneo hili ambapo ni moja ya chanzo cha Mto Ruaha kilichopo katika Kijiji cha Kikondo eneo linalotenganisha eneo la Hifadhi ya Taifa ya Kitulo  yametolewa mapendekezo kuwa wananchi waliopo katika eneo hili waondoke na kupisha chanzo hicho cha maji.

Akizungumza wakati akiukaribisha ugeni huo, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka amesema, eneo hilo limekuwa likifanyika shughuli mbalimbali za kilimo na hivyo kuwa chanzo kikuu cha shughuli za uzalishaji kwa wananchi hao.

Mwenyekiti anayeongoza timu hiyo,  Doroth Mwanyika ambaye ni Katibu mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi  amesema kwa sasa watawasilisha taarifa walizokusanya kwa  mawaziri na baadaye kutafuta namna nzuri ya kutekeleza mapendekezo yatakayosaidia kulinda chanzo hicho kwa maendeleo ya siku zijazo.

Mwanyika amesema, walichokibaini kwanza hakukuwa na mgogoro wowote wa mpaka ila walikiona ni hatari iliyopo kutokana na mto Ruaha kutegemewa kutiririsha maji yake katika Mto Rufiji ambao unatarajiwa kuzalisha umeme kupitia mradi mkubwa uliotangazwa na serikali hivyo kuathirika kwake kutaleta madhara kwa kiwango kikubwa.

Makatibu wakuu waliopo  katika timu hiyo ni wa wizara ya  ardhi nyumba na maendeleo ya makazi,  Wizara ya  Maliasili na Utalii, pia katibu Wizara ya Katiba na Sheria.,  katibu Mkuu Wizara ya Maji akiwemo pia  Katibu mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na katibu mkuu ofisi ya0000 Rais  Tamisemi.

Serikali yazuia shilingi bilioni 5.5 za ujenzi wa soko Kinondoni

Serikali imezuia Shilingi bilioni 5.5 ambazo zilipaswa kutumika kutekeleza mradi wa Kimkakati wa Soko la Magomeni liliko wilayani Kinondoni Jijini Dar es Salaam kutokana na kucheleweshwa kwa utekelezaji wa mradi huo licha ya kupewa fedha za kutosha kwa awamu ya kwanza.

Hatua hiyo imechukuliwa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji baada ya kutembelea na kukagua ujenzi wa mradi huo unaotarajia kugharimu shilingi bilioni TISA (9) na kukuta ujenzi wake unasuasua.

Dkt. Kijaji alisema kuwa Serikali, imeipatia Manispaa ya Kinondoni shilingi bilioni 3.5 tangu mwezi Mei, 2018 kwa ajili ya kutekeleza mradi huo ambao ungepaswa ukamilike ndani ya miezi tisa tangu kusainiwa kwa mkataba wa ruzuku hiyo lakini ameshangaa kutomkuta mkandarasi kwenye eneo la ujenzi.

Awali, akitoa maelezo ya mradi huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Kinondoni, Mhandisi wa Manispaa hiyo, Justin Lukaza, ameeleza kuwa Manispaa hiyo imeingia mkataba wa kujenga soko hilo litakalokuwa na ghorofa tatu na Kampuni ya Group Six International na kwamba ujenzi wa mradi huo ungekamilika katika kipindi cha miezi sita ijayo na kutofautiana maelezo na Mkandarasi ambaye alimweleza Dkt. Kijaji kuwa ujenzi huo ungechukua muda wa  miezi 12.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo, amekiri kuwepo na uzembe uliofanywa na watendaji wa Manispaa ya Kinondoni uliosababisha mradi huo kuchelewa kuanza na kumwomba Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji kumpatia muda mfupi wa kurekebisha kasoro hizo.

Chongolo amesema kuwa tayari kuna hatua mbalimbali zilizochukuliwa kwa maafisa waliofanya uzembe katika utekelezaji wa mradi awali na hakujua kama bado kulikuwa na uzembe uliokuwa unaendelea baada ya kuchukua hatua hizo kwa sababu aliamini watendaji waliokabidhiwa kusimamia ujenzi wa mradi huo walijifunza kutokana na makosa ya wenzao walioondolewa kusimamia mradi huo.

Mradi wa Soko la Kisasa la Magomeni ni miongoni mwa miradi 22 iliyopewa ruzuku na Serikali katika Mpango wa Awamu ya Kwanza wa kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kujitegemea kimapato ambapo zaidi ya shilingi bilioni 147 zilitolewa na Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo.

Rais Magufuli afanya uteuzi mwingine

Rais John Magufuli amemteua Dkt. Michael Wilfred Ng’umbi kuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW).

Kabla ya uteuzi huo Dkt. Ng’umbi alikuwa Mhadhiri Mwandamizi wa Kitivo cha Elimu cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, uteuzi wa viongozi hao umeanza leo, Jumatano Februari,19.

Dkt. Ng’umbi amechukua nafasi ya Dkt. Fidelice Mafumiko ambaye ameteuliwa kuwa Mkemia Mkuu wa Serikali.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amemteua Jaji Stephen Mrimi Magoiga kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Ushindani (Fair Competition Tribunal – FCT)

Jaji Magoiga amechukua nafasi ya Jaji Barke Mbaraka Sehel ambaye ameteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.

Serikali yasisitiza haitawalipa 'Kangomba'

Sheria ya Korosho Kifungu cha 12 hakimruhusu mtu yeyote kufanya kazi ya korosho pasi na kutambulika, wakati kifungu cha 15 cha sheria hiyo katika kifungu kidogo cha nne kinawataka wahusika wote wa korosho wawe wamesajiliwa na kuwa na leseni ya biashara hiyo.

Bila kuwa na usajili huo kwa mfanyabiashara yeyote wa korosho ni kosa kisheria hivyo kwa atakayebainika anapaswa kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Kufuatia vifungu hivyo vya sheria, Serikali imetilia mkazo maagizo iliyoyatoa hivi karibuni kuwa katika malipo ya wakulima wa korosho haitamlipa mfanyabiashara asiyetambulika kisheria (Kangomba).

Hayo yamesemwa jana, Jumanne 19 na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga alipotembelea    Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga na kuzungumza na madiwani wa mkoani Pwani.

Waziri Hasunga amesema kuwa ni lazima sheria zifuatwe katika utekelezaji wa majukumu yote ikiwemo biashara ya zao la korosho ili kuwanusuru wakulima wanaotumia nguvu nyingi katika kilimo hicho huku wakipata matokeo duni kutokana na baadhi ya wafanyabiashara wanaowahujumu (Kangomba).

Ameongeza kuwa wahujumu katika biashara za mazao mbalimbali ya kilimo nchini katika kipindi kirefu wamekuwa wakiwanyanyasa wakulima kwa kuwanyonya katika bei jambo ambalo serikali imelibaini na hivyo kuingilia kati.

Akizungumzia sababu ya wakulima kuchelewa kulipwa fedha za korosho zao, Hasunga amesema imetokana na uhakiki kuchukua muda mrefu uliosababishwa na vyama vya Ushirika kutofanya kazi yao ipasavyo kwa kuwasajili na kuwatambua wakulima.

“Vyama vya ushirika ndivyo vinapaswa kuwajua na kuwatambua wakulima wake katika mazao yote yanayouzwa kupitia mfumo huo, vinginevyo kutofanya kazi kwa weledi kumetuchelewesha kwa kiasi kikubwa,” alikaririwa Hasunga na kuongeza kuwa

“Hata sheria yetu ya maghala haikufanya kazi vizuri, Vyama vya Msingi havikutekeleza majukumu yake.”

Aidha waziri Hasunga ameonya kuwa serikali haitawavumilia wote wanaofanya biashara hiyo kinyume na sheria badala yake watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufunguliwa kesi za uhujumu uchumi.

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga yuko katika ziara ya kikazi mkoani Pwani, Lindi na Mtwara ambapo katika ziara hiyo anafuatilia mwenendo wa malipo ya wakulima wa zao la korosho.

Serikali yashauriwa kuongeza bajeti ya masuala ya watoto

Wadau wameishauri Serikali kuongeza kiwango cha Bajeti katika masuala yahusuyo maendeleo na ustawi wa mtoto ili kuwezesha mipango mbalimbali kutekelezeka katika kumpatia mtoto haki na ustawi wake.

Hayo yamebainika leo jijini Dodoma katika kikao kilichowakutanisha Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Mashirika ya C-SEMA na SOS-Children Village Tanzania kujadili jinsi ya kuweka mikakati madhubuti katika kuwezesha ongezeko la Bajeti katika masuala ya watoto nchini.

Akitoa taarifa ya utafiti huo Mwakilishi wa Shirika la SOS-Children Tanzania, Mpelly Ally amesema kuwa utafiti huo uliofanyika katika mwaka wa fedha 2015/16 na 2017/2018 umeonesha kuwa kwa kiasi kikubwa fedha zilizotengwa katika Bajeti ya Wizara husika kwa ajili ya masuala ya watoto hakikutolewa na zilizotolewa zilikuwa kwa asilimia ndogo kabisa kuweza kutekeleza afua mbalimbali za watoto nchini.

Ameongeza kuwa mara baada ya kupata matokeo hayo na kubaini kuwa kuna upungufu wa Bajeti katika masuala ya watoto waliamua kuja na mapendekezo kadhaa ikiwemo Serikali kuisambaza hiyo taarifa kwa wadau mbalimbali wa maendeleo ili kuona jinsia watakavyosaidia kuwezesha kuondokana na upungufu huo.

Ameyataja mapendekezo mengine kuwa Wizara kutoa elimu kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ili kuweza kujua umuhimu wa kutenga na kuwezesha utoaji wa fedha kwa ajili ya masuala ya  maendeleo na ustawi wa mtoto nchini.

“Kikubwa tunaishauri Serikali iyafanyie kazi mapendekezo yetu ili tuhakikishe mtoto haachwi nyuma kufikia maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030”alisema

Akichangia katika kikao hicho Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Patrick Golwike amesema kuwa ili kuipa nguvu tafiti hiyo wadau hao wanapaswa kuja na sababu yenye mashiko zaidi ya kwanini kuongezeka kwa Bajeti ya mtoto ili kuisaidia Serikali kupambanua na kuja na mikakati madhubuti.

Naye Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Jinsia, Julius Mbilinyi amewataka wadau hao kuja na orodha ya mahitaji na wapi kunahitajika, ongezeko la Bajeti katika masuala ya mtoto nchini ili kuwepo na uelewa wa pamoja wa Serikali na wadau katika kulitekeleza hilo.