Maduro atangaza utayari wa kijeshi dhidi ya Marekani

|
Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro akikagua utayari wa vikosi vya jeshi dhidi ya Marekani

Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro amejitokeza katika Televisheni ya Taifa na kutangaza utayari wa jeshi lake kukabiliana na aina yoyote ya uvamizi ama mashambulizi ya Marekani dhidi ya nchi hiyo.

Kauli ya Maduro imekuja baada ya kutembelea viunga vya mazoezi ya kijeshi akiambatana na waziri wa Ulinzi na makamu wa Rais katika Jimbo la Miranda nchini Venezuela.

Mazoezi hayo ya kivita yamehusisha majaribio ya mifumo ya kudhibiti mashambulizi kutoka angani na silaha nyingine za kivita, lakini Maduro amesema bado majaribio muhimu hayajafanyika. 

“Vitisho vya Marekani vimetulazimisha kujiandaa kwa uhakika ili kulinda haki na amani ya nchi, kulinda utu wa watu wa Venezuela, uhuru kamili kama Taifa, kulinda uhuru wa kuishi katik karne hii ya 21 kama Taifa huru lenye watu huru.” Alisema Maduro.

Kiongozi huyo wa kisoshalisti anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Kiongozi wa Upinzani,  Juan Guaido kijana mwenye umri wa miaka 35 na Raisi wa Kambi ya upinzani Bungeni aliyejitangaza kuwa Rais wa mpito nchini Venezuela mwishoni mwa mwezi Januari mwaka huu.

Licha ya shinikizo la kuondoka madarakani kwa madai ya kushinda isivyo halali katika uchaguzi uliomweka madarakani, lakini Maduro ameshikilia msimamo wake wazi kwamba hataondoka madarakani kirahisi.

Guaido ameomba msaada wa kibinadamu kama dawa na chakula kutoka mataifa yanayomuunga mkono, lakini Maduro amekataa misaada hiyo kuingia nchini humo kwa madai kuwa Venezuela sio ombaomba.

Utawala
Maoni