Mahakama Kuu yatupilia mbali ombi la Serikali

|
Wanasiasa wa vyma vya upinzani waliofungua kesi mahakama kuu

Mahakama kuu Jijini Dar es Salaam imetupilia mbali ombi la upande wa Serikali la kutaka wapewe siku 21 za kujibu hoja za upande wa walalamikaji kuhusu Muswada wa Vyama vya Siasa Nchini uliowasilishwa mahakamani hapo na Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe na wenzake wawili.

Mahakama katika shauri hilo imekubaliana na hoja ya upande wa waombaji ya kuomba kupunguza siku za serikali kujibu hoja walizowasilisha ili kesi isikilizwe kabla ya muswada haujasomwa kwa mara ya pili bungeni na kuzingatia kuwa shauri hilo limelenga maslahi ya umma.

Hoja zilizowasilishwa mahamakani hapo na upande wa watoa hoja ni mosi, Muswada kuwa na mushkeli lakini pili ni kuomba zuio la muswada kujadiliwa bungeni kama walivyoomba ambapo mahakama kuu imetoa siku saba badala ya siku 21 zilioombwa na Jamhuri na hivyo shauri hilo litaletwa tena Ijumaa ijayo kwa kusikilizwa.

Shauri hilo limendeshwa na jopo la majaji watatu ambao ni Jaji Barke Sahel, Jaji Salima Magimbi na Jaji Ben Hjji huku upande wa Serikali ukiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Mark Muruambo na Wakili  Rehema Mtuliya wakati kwa upande wa utetezi ukiendeshwa na Wakili Stephen Mwakibolwa na Wakili Fedrick Kiwelo.

Shauri hilo lilifunguliwa rasmi Mahakama Kuu ya Tanzania Januari 12, mwaka jana.

Mahakamani
Maoni