Mahakama Zambia yamsafishia njia Rais Lungu 2021

|
Rais wa Zambia, Edgar Lungu aliyeruhusiwa na Mahakama ya Kikatiba ya nchi hiyo kuwania urais 2021

Mahakama ya Kikatiba ya Zambia imesema Rais wa sasa wa nchi hiyo, Edgar Lungu anazo sifa za kuwania nafasi hiyo tena katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2021.

Uamuzi huo wa Mahakama umetangazwa leo, Ijumaa na hivyo kutupilia mbali hoja ya wapinzani waliotaka Lungu asiwanie tena urais wakidai tayari ameshahudumu kwa awamu mbili kwa mujibu wa Katiba.

Wafuasi wa Chama cha Patriotic Front cha Rais, Edgar Lungu walifika mahakamani hapo wakiwa na shauku ya kutaka kujua uamuzi wa Mahakama hiyo mjini Lusaka.

Hata hivyo wengi wao walikuwa wamejawa na furaha tayari tangu awali kabla ya uamuzi huo kutolewa na  kunogeshwa zaidi na waliokuwa ndani ya Mahakama baada ya hukumu hiyo.

"Mahakama ya Kikatiba imeliweka vyema suala hili, imesema Rais Edgar Lungu anazo sifa za kuwania mwaka 2021."

"Hoja ilikuwa ni kwamba je vipindi viwili alivyovitumikia vinakamilisha awamu mbili za uongozi wake kwa mujibu wa Katiba? Jibu la Mahakama ni kwamba, si kweli."

Lakini ni nini kimetokea nchini Zambia?

Mwaka 2014 mwezi Oktoba Zambia ilimpoteza Rais wake wa Tano marehemu, Michael Charles Chilufya Sata aliyekuwa ameiongoza nchi hiyo kwa awamu moja kuanzia mwezi Septemba mwaka 2011.

Kutokana na kifo hicho uliitishwa uchaguzi wa mwezi Januari mwaka 2015 ambapo Edgar Lungu alishinda na kuhudumu kwa mwaka mmoja na nusu kabla ya uchaguzi mkuu wa mwezi Agosti mwaka 2016 ambapo alishinda tena na kuwa madarakani mpaka sasa.

Mwaka jana Lungu alitangaza rasmi kuwania uchaguzi wa mwaka 2021 na ndipo baadhi ya vyama upinzani na chama cha wanasheria wakaenda kwenye mahakama ya Katiba wakimpinga kwa hoja kuwa Rais huyo anavunja Katiba kwa kuwania awamu ya tatu.

Jaji wa Mahakama ya Katiba, Hildah Chibomba amesema urais wa awali wa Lungu wa mwaka mmoja na nusu hauwezi kuhesabiwa kuwa ni awamu iliyotimia.

Hukumu
Maoni