Majaliwa awatoa hofu wakulima wa korosho nchini

|
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua namna korosho zinavyobanguliwa katika Kiwanda cha korosho cha Terra

Waziri mkuu, Kassim Majaliwa amewatoa hofu wananchi hususan wakulima wa korosho nchini baada ya kuwahakikishia kuwa korosho zao zote zitanunuliwa.

Amesema Serikali kupitia Bodi ya Mazao Mchanganyiko itanunua korosho zote na hakuna korosho za wakulima nchini ambazo zitabaki bila ya kununuliwa.

Ameyasema hayo leo Ijumaa, Desemba 7, alipozungumza na wafanyakazi wa Kiwanda cha Korosho cha Terra akiwa njiani kwenda Dodoma.

Waziri Mkuu amesema bodi hiyo inaendelea kufanya thamini na kujiridhisha kama kweli korosho hizo zimezalishwa nchini na kuangalia viwango vya ubora.

Amesema baada ya kujiridhisha kuhusu viwango vya ubora na mkulima aliyepeleka ndiye mwenyewe ndipo taratibu za malipo hufanyika.

Waziri mkuu amesema kuwa Serikali iliamua kununua korosho zote baada ya wafanyabiashara kutaka kuzinunua kwa bei ya chini ambayo haikuwa na tija.

“Lengo la Serikali ni kuhakikisha mkulima ananufaika na ndipo Rais Dkt. John Magufuli alisitisha ununuzi baada ya kuona wakulima wanataka kudhulumiwa.”

Waziri Mkuu amesema kuwa hadi sasa tayari tani 181,000 zimeshakusanywa, hivyo amewataka wakulima wa zao hilo nchini waendelee kuiamini Serikali yao.

Wakati huo huo Waziri Mkuu ameupongeza uongozi wa kiwanda hicho kwa kuunga mkono jitihada za Serikali kukuza uchumi kwa kupitia sekta ya viwanda.

Awali, Meneja Utawala wa Kiwanda cha Terra, Peter Ngwale alisema uwezo wao ni kubangua tani 6,000 kwa mwaka, ambapo tayari wameshabangua tano 3,000.

Meneja huyo aliiomba Serikali iwasaidie katika suala la ubora wa korosho kwa kuwa kiwango cha ubora kinachoandikwa kinapowasilishwa kiwanda ni tofauti na uhalisia wa korosho  yenyewe.

Biashara
Maoni