Makamu wa Rais awataka Watanzania wanaoishi nje kuwekeza nchini

|
Watanzania waishio Uganda walipokutana na kuzungumza na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan nchini Uganda

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inayoongozwa na Rais Magufuli pamoja na wasaidizi wake imeamua kufanya kazi kwa bidii kwa lengo la kukuza uchumi.

Makamu wa Rais ameyasema hayo alipokutana na viongozi wa Watanzania wanaoishi nchini Uganda katika Hoteli ya Munyonyo Commonwealth Resort jijini Kampala.

“Katika kuleta uchumi wa viwanda, Serikali imedhamiria kuongeza na kuboresha upatikanaji wa Umeme, huduma ya maji, kuboresha mitaala ya elimu,kuboresha huduma za afya pamoja na miundombinu.” Alisema makamu wa Rais.

Makamu wa Rais amewaambia viongozi hao wa Watanzania wanaoishi nchini Uganda kuwa miradi mingi inayofanyika Tanzania kwa sasa inafanyika kwa kutumia fedha za ndani.

Pamoja na mambo mengine, Makamu wa Rais amewataka Watanzania waishio nje ya nchi  kuwekeza nchini kwani kuna maboresho mengi ya kuvutia wawekezaji yamefanyika.

Kwa upande wake,  Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro amesema kuna Watanzania zaidi ya milioni mbili (2) wanaishi nchi za nje hivyo amewaomba kuwa mabalozi wazuri wa kuisemea nchi yao.

Katika kuhitimisha mkutano wa Africa Now Summit 2019, Makamu wa Rais alipata nafasi ya kuchangia katika suala zima la mtazamo wa kijinsia ambapo alisema bado wanawake hawapewi nafasi ya kutosha kwenye mambo mengi ya msingi kuanzia kwenye elimu, uongozi na masuala mengine ya huduma za kijamii.

Makamu wa Rais pia alizungumzia suala zima la wanawake wanaofanya biashara za mipakani kuwa wamekuwa wakinyanyasika na kuna wakati wanaonekana ni watu wa kupitisha magendo hivyo kushauri mamlaka husika kutambua na kusaidia wanawake hao ambao ni vinara wa kuhudumia  familia na jamii nzima.

Makamu wa Rais alikutana pia na kufanya mazungumzo na Rais wa Uganda, Yoweri Museven.

Utawala
Maoni