Marekani yapeleka wanajeshi DRC kwa tahadhari ya kuzuka vurugu za uchaguzi

|
Rais wa Marekani, Donald Trump amesema ataongeza wanajeshi wengine iwapo 'atalazimika' kufanya hivyo.

Serikali ya Marekani imepeleka wanajeshi wake 80 nchini Gabon kwa tahadhari ya kutokea maandamano ya vurugu wakati matokeo ya uchaguzi wa rais wa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) yatakapotangazwa.

Matokeo ya Rais wa DRC yanatarajiwa kutangazwa siku ya Jumapili ingawa Tume ya Uchaguzi nchini humo (CENI) ilishatoa tahadhari huenda matokeo hayo yakachelewa kutangazwa kutokana na kufika pole pole kwa fomu za matokeo kutoka vituo vya kupigia kura.

Kwenye barua yake kwa viongozi wa Congress, Rais Donald Trump amesema anaweza akaongeza wanajeshi zaidi “iwapo italazimika”.

Amesema ‘watabaki huko hadi hali ya amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo itakapoonyesha kuwa uwepo wao huko hauhitajiki tena.’

Tume ya Uchaguzi nchini Congo inatarajiwa kutangaza matokeo ya awali ya Rais na wabunge siku ya Jumapili ingawa ilisema huenda matokeo hayo yakachelewa kutangazwa kwa sababu yanafika kwenye ofisi za tume ‘pole pole’.

Waangalizi na vyama vya upinzani wamesema uchaguzi huo uligubikwa na ukiukwaji wa taratibu nyingi.

Serikali ya Congo imesema uchaguzi ulienda vizuri.

Jumuiya ya kimataifa imeonya kuwa matokeo ambayo hayatakubalika yanaweza kuzua vurugu kama ilivyotokea kwenye uchaguzi wa mwaka 2006 na 2011.

Siku ya Alhamisi wizara ya Mambo ya Ndani ya Marekani iliitaka CENI kuhakikisha kura zote zinahesabiwa kwa usahihi na ikatishia kuwawekea vikwazo watu watakaokwamisha mchakato huo au kutishia amani na ustawi wa taifa hilo (DRC).

Maisha
Maoni