Mbowe na Matiko wakwama tena mahakama Kuu

|
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe akiwa na Mbunge wa Tarime mjini, Ester Matiko wakiwa Mahakama Kuu kusikiliza rufaa yao

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda  ya Dar es Salaam imesitisha usikilizwaji wa rufaa ya Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe pamoja na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko  hadi pale ambapo uamuzi wa rufaa iliyowekwa na upande wa Jamhuri itakapotolewa.

Uamuzi huo umetolewa na Jaji Sam Rumanyika  kufuatia uamuzi wa upande wa mashtaka  kuchukua hatua za kukata rufaa ya kupinga uamuzi  uliotolewa na Mahakama kuu ambayo iliiona pingamizi lililowekwa na Jamhuri halina msingi na hivyo leo upande huo kuchukua hatua za kukata rufaa ya kupinga maamuzi yaliyotolewa na mahakama hiyo ya kuachana na hoja yao.

Upande wa  Jamhuri unaongozwa na jopo la mawakili wannne akiongozwa na Wakili mkuu wa Serikali, Faraja Nchimbi  na Paul Kadushi  huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na jopo la mawakili wanane chini ya Peter Kibatala.

Katika uamuzi huo Jaji Rumanyika amekubaliana na hoja za upande wa Jamhuri ya kuwa uamuzi mdogo hauwezi kumaliza shauri, pia hauwezi kukatiwa rufaa na mtu mwingine yeyote isipokuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Kuhusu suala la kusudio la Rufaa, Jaji Rumanyika amesema kuwa  kunapokuwa na  taarifa ya kusudio la kukata  rufaa mahakama ya chini haiwezi kuendelea na shauri,  hivyo  mwenendo wa kusikiliza rufaa hiyo utasitishwa hadi pale ambapo Mahakama ya  Rufaa itakapotoa uamuzi wa rufaa iliyokatwa na upande wa Jamhuri.

Washtakiwa hao wawili walifutiwa dhamana Novemba 23, mwaka huu  na Hakimu mkazi mkuu wa Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu, Wilibard Mashauri  kwa madai ya kukiuka mashrti ya dhaman hiyo.

Katika  kesi ya msingi iliyopo katika Mahakama ya hakimu mkazi Kisutu, Mbowe na wenzake wanakabiliwa na jumla ya mastaka 13 likwemo la kufanya mkusanyiko usio halali.

Mahakamani
Maoni