Meya wa Mikindani na diwani wajiunga CCM

|
Aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Mikindani Mtwara Mjini kwa tiketi ya CUF, Jofrey Mwanchisye baada ya kujiuzulu na kujiunga CCM

Aliyekuwa Diwani wa Kata ya Tandika na Meya wa Manispaa ya Mikindani Mtwara Mjini, Jofrey Mwanchisye amejiuzulu nyadhifa hizo na kujiunga na CCM.

Mbali na Mwanchisye, Diwani mwingine wa Kata ya Chikongola wilayani humo Mussa Namtema naye amejiuzulu wadhifa huo na kujiunga na chama hicho.

Mwanachisye na Namtema wametangaza uamuzi huo, leo Jumatano Machi 27, 2019 katika ofisi za CCM Mtwara Mjini zilizopo Kata ya Raha leo, Jumatano.

Hatua ya Mwanchisye imekuja baada ya kupita siku tano tangu ajiuzulu aliyekuwa Meya wa Ilala na Diwani wa Bonyokwa (Chadema), Charles Kuyeko.

Meya huyo amedai kuwa amechukua uamuzi wa kujiunga na CCM baada ya kuridhishwa na utendaji kazi wa Rais John Magufuli.

“Nilichokifanya siyo dhambi ni jambo la kawaida hasa ukiona huridhishwi na masuala yanavyokwenda katika chama ulichokuwa,” amesema na kuongeza kuwa anakwenda CCM kwa sababu ni salama. Kwa upande wake Namtema amesema naye amejiuzulu ili kujiunga na CCM kuunga mkono utendaji wa Rais Magufuli.

Alipotafutwa Naibu Katibu wa CUF Bara, Magdalena Sakaya amesema bado hajapata taarifa hizo huku akiahidi kuifuatilia kwa kina ili apate uhakika.

Mbali na Sakaya, mwingine aliyetafutwa ni Makamu Mwenyekiti CUF Bara, Maftaha Nachuma ambaye pia ni mbunge wa Mtwara Mjini aliyesema hana taarifa, ingawa amezikisikia na kuziona kwenye mitandao ya kijamii.

Utawala
Maoni