Mgomo wa daladala Manyara waathiri shughuli muhimu

|
Abiria wakitumia usafiri wa vigari vya mizigo kufika wanakoenda baada ya daladala kugoma

Wakazi wa  maeneo ya  Galapo  wilayani Babati mkoani Manyara wameshindwa kupata huduma ya usafiri kwa muda wa siku mbili jana na leo,  kutokana na watoa huduma hiyo maarufu kama daladala kusitisha huduma hiyo, kutokana na kile wanachokidai kuwa umbali wa safari umeongezeka kutokea stendi mpya hadi kufika Galapo na kuamua kupandisha nauli kutoka shilingi 1000 hadi 1500.

Azam News ilifanikiwa kufika katika stendi mpya ya mabasi na daladala iliyopo Makatanini ndani ya Halmashauri ya mji wa Babati na kushuhudia abiria wakiwa hawana la kufanya baada ya daladala hizo za Galapo kusitisha safari kwa muda usiojulikana.

Akizungumzia sakata hilo Katibu mkuu wa wamiliki wa mabasi Mkoa wa Manyara (MABOA)  Omary Chaka aliyedai kuwa umbali wa eneo ambako kituo kimepelekwa mbali na hivyo kuwaongezea gharama.

Kwa upande wake, Afisa mfawidhi SUMATRA Mkoa wa Manyara, amesisitiza kuendelea kutumika kwa nauli za awali na kwamba Mkurugenzi mkuu wa SUMATRA Tanzania ndiye mwenye mamlaka ya kutangaza ongezeko la nauli.

Stendi mpya ya mabasi na daladala iliyopo Makatanini ilianza rasmi kutumika Januari Mosi mwaka huu.

Usafiri
Maoni