Misaada yaanza kuwafikia waathirika wa kimbunga Idai

|
Baadhi ya wakazi wa maeneo ambayo Kimbunga Idai kimeathiri nchini Msumbuji wakipokea misaada mbalimbali baada ya kushindikana awali

Misaada ya kibinadamu kwa walioathiriwa na kimbunga Idai nchini Msumbiji imeanza kuwafikia watu wengi zaidi baada ya maji ya mafuriko kuanza kupungua tangu yalipoyazonga makazi kwa zaidi ya wiki na kuathiri zaidi ya watu milioni moja.

Hayo yanatokea wakati tathmini ya athari za kimbunga Idai ikiendelea nchini Msumbiji huku pia baadhi ya barabara zikiwa zinakarabatiwa hali ambayo inarahisisha zaidi huduma za uokoaji na usambazaji wa chakula, dawa, maji na mavazi.

Wakati misaada hiyo ikiendelea kusambazwa, Shirika la Msaada Mwekundu limewataka waokoaji kuchukua tahadhari zaidi kutokana na tishio la magonjwa ya mlipuko katika maeneo yaliyoathiriwa na kimbunga Idai.

Nchini Msumbiji pekee zaidi ya watu 400 wamefariki dunia kutokana na kimbunga Idai ambacho kimesababisha pia vifo katika mataifa ya Zimbabwe na Malawi.

Zaidi ya watu milioni mbili wameathiriwa na kimbunga Idai katika nchi za Msumbiji, Zimbabwe na Malawi huku mamia ya watu wakiwa hawajulikani walipo mpaka sasa hali inayozidisha hofu zaidi ya kuongezeka kwa vifo.

Vimbunga
Maoni