Mkapa aamua kupumzika kutatua mgogoro wa Burundi

|
Rais mstaafu wa awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa aliyekuwa pia msuluhishi wa mgogoro wa kisiasa wa Burundi

Rais Mstaafu wa awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ameachia ngazi nafasi ya kuendelea kuwa msuluhishi katika mazungumzo ya kutatua mzozo wa kisiasa nchini Burundi, msemaji wake ameieleza BBC.

Mgogoro huo wa kisiasa ulipamba moto mwaka 2015 baada ya Rais wa sasa Pierre Nkurunziza kujiongeza muhula wa tatu ulioleta sintofahamu nchini humo na kupingwa vikali na upinzani.

"Kipindi cha kusuluhisha kimefikia mwisho,’’alinukuliwa akisema Makocha Tembele.

Hata hivyo msemaji huyo amekanusha kuwepo kwa taarifa zinazodai kuwa Rais Mkapa amejiuzulu nafasi hiyo.

"Ni mwisho wa mamlaka yake," alisema, na kuongeza kuwa Mkapa ameshawasilisha ripoti yake ya mwisho wakati wa mkutano wa mwisho wa viongozi wakuu wa nchi za Afrika Mashariki uliofanyika mapema mwezi huu.

Tembele amesema kilichobaki ni kwa upande wake Rais wa Uganda, Yoweri Museveni kuendelea na awamu inayofuata ya usuluhishi ambayo inapaswa kufanyika kabla ya uchaguzi ujao unaotarajiwa kufanyika mwakani.

Hata hivyo mazungumzo hayo yalitokana na vurugu zilizotokea nchini humo na kuuawa watu takribani 1,000 yanaonekana kutofanikiwa kutokana na Serikali kwa mara kadhaa kugomea kutuma ujumbe katika vikao vinavyoitishwa na wasuluhishi hao.

Utawala
Maoni